Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Watakaoshindwa kutekeleza ilani ya CCM kuachia ngazi

 


Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe, Jessen Mwamala amewataka watendaji walioteuliwa na raisi Samia Suluhu Hassan ambao watashindwa kutekeleza ipasavyo ilani ya chama hicho kuachia nafasi hizo.


Kauli hiyo ameitoa  kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika ukumbi wa halmashauri ya mji mkoani hapa.


Amesema chama hicho kinategemea kuwa utendaji wao kulingana na nafasi zao watatekeleza vizuri ilani ya chama hicho cha kuwaletea maendeleo wananchi.


Alisema iwapo watendaji hao watatekeleza vizuri ilani ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kitafanya vizuri kwa viongozi wake kuchaguliwa kwa mara nyingine tena.


"Tumekuwa tukisema ukiona wewe ilani hii ni ngumu kwako sijui tuseme ujiondoe au utuachie nafasi hiyo" alisema Mwamala.


Amesema kuteuliwa kwao Raisi Samia ameangalia vitu vingi ikiwemo uwezo wa kufanya kazi na kuleta maendeleo kwa wananchi.


Amesema chama hicho kina kazi ya kuhakikisha yale yaliyoahidiwa na chama hicho yanatekelezwa na pia kuondoa kero ambazo zinawakabili wananchi.


"Tukafanye kazi kulingana na haya mafungu ya fedha zilizoletwa siyo tuzile bali zifanye kazi ambazo mkuu wetu wa mkoa alizozitaja" alisema Mwamala.


Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya amesem mkoa umepokea Sh 1.9 bilioni zinazotolewa na tozo za miamala ya simu kwa ajili ya ukamilishaji wa miundo mbinu ya sekondari na ujenzi wa vituo vya afya.


Alisema kwa upande wa barabara vijijini bajeti ya matengenezo na ujenzi wa miradi mipya imeongezeka kwa kiasi kikubwa.


" Katika bajeti ya fedha kwa mwaka uliokwisha tulikuwa na bajeti ya Sh8.4 bilioni lakini mwaka huu wa fedha bajeti ya matengenezo na miradi ya maendeleo zinafikia 20. 2 ni ongezeko karibu mara mbili ya bajeti ya mwaka jana" alisema Rubirya.

Post a Comment

0 Comments