Mtanzania wa kwanza kuchezesha soka Uingereza

Ericsson Temu ni mwamuzi wa soka anayechezesha soka nchini Uingereza na kuwa ndio Mtanzania wa kwanza kuchezesha soka nchini humo.

Temu aliweka historia ya kipekee ya kuwa mwamuzi wa kwanza mtanzania kuchezesha soka nchini England, alipochezesha pambano baina ya Charlton Athletics FC dhidi ya Queens Park Rangers FC kwa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 23.

Katika kipindi cha majuma matatu ya mwezi Desemba, Mtanzania huyu amechezesha michezo iliyohusisha Arsenal U20 dhidi ya Southend United U20, Crystal Palace U20 dhidi ya Stevenage FC U20, pia akichezesha mchezo MK Dons U20 dhidi Crystal Palace U20,

Pia Mwamuzi huyu amechezesha mchezo wa Kombe la Shirikisho kwa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 23 aliposimamia mchezo wa raudi ya tatu kati ya Herne Bay FC dhidi ya Catford Wanderers (2008).

Temu aliangukia katika uamuzi baada ya kukosa nafasi kwenye soka hivyo alilazimika kuachana na uchezaji wa soka na kutimkia kwenye taaluma ya uamuzi ambapo alianza taaluma hiyo mnamo mwaka 2009 jijini Arusha baada ya kusomea kozi maalumu za uamuzi zilizokuwa zikitolewa na Chama cha Soka Mkoa wa Arusha.

Mwaka 2016 alienda nchini Mauritius kwa masomo ya chuo kikuu na aliendelea na mapenzi yake ya kuchezesha soka ambapo alifanikiwa kuchezesha michezo takribani 194 kwenye madaraja mbali mbali ikiwemo ya Daraja la I, II, III, National League pamoja na michezo ya Kombe la Shirikisho (FA).

Kujiunga na Shirikisho la Soka la Mauritius kulimfanya kuwa mwamuzi wa kwanza Mtanzania kuchezesha michezo ya ligi ya ndani (Domestic Leagues) kwenye taifa la kigeni nje ya Tanzania. Kwa nyakati tofauti kati ya 2016 hadi 2020, Ericsson alipata fursa ya kualikwa na kuchezesha kwenye mashindano madogo ya ndani barani Ulaya na Asia.

Akizungumza na BBC , Ericsson anasema kuwa ''Kufanya kazi kama mwamuzi imekuwa safari ya kusisimua nimejifunza mengi kutoka kwa wataalamu, ndani na nje ya nchi. Ninaweza kusema kila mwamuzi ambaye ameamua kuacha wakati wake kuchukua kazi hii ni bora. Huwezi kuondoa sifa kwa aliyekuwa mwamuzi wa FIFA Mtanzania Bw Othman Kazi. Hatahivyo, hakuna mwamuzi aliyenikosha kama Pierluigi Collina. Binafsi, Collina ni hadithi inayoishi; mwamuzi Bora wa Mwaka" wa FIFA mara sita mfululizo, ni mara kwa mara kuona mtu akidumisha hadhi kama hiyo kwa zaidi ya miaka sita, lakini alifanya hivyo''.

Mwamuzi huyu kijana ana ndoto kubwa ya kuchezesha ligi kuu ya England na michuano ya kombe la dunia ''kwangu ni zaidi ya ndoto au hamu, kwangu ni lengo na msukumo kuwa siku moja kwa kudra za Mwenyezi Mungu kuchezesha Kombe la Dunia la FIFA''. Aliiambia BBC.

 

Post a Comment

0 Comments