Zuhura Yunus kuondoka BBC

 


Mtangazaji mashuhuri wa BBC Zuhura Yunus anaondoka kutoka shirika hilo baada ya kulitumikia kwa takriban miaka 14 .


Zuhura atatangaza kipindi chake cha mwisho cha Dira ya Dunia majira ya saa tatu Afrika mashariki .


Hata hivyo amebakiza siku kadhaa za likizo kabla ya kuondoka rasmi.


Mtangazaji huyo aliyejiunga na BBC Swahili mwaka 2008 amesema anataka kuutumia muda wake sasa kuendelea na uandishi na mambo mengine nje ya BBC.


Taarifa ya Zuhura kuondoka BBC inakuja miezi kadhaa baada ya kuandika kitabu chake cha wasifu wa Biubwa Amour Zahor mwanaharakati mwanamke wa kisiasa wakati wa mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.


Zuhura alianza kama mtangazaji wa redio na mzalishaji wa vipindi mwaka 2008. Mwaka 2014 alihamia Swahili TV na akawa mwanamke wa kwanza kutangaza Dira ya Dunia TV.


Wakati wote huo Zuhura alichangia pakubwa kufanikisha vipindi vilivyo peperushwa kwenye redio na runinga ikiwemo wakati wa uchaguzi wa Marekani mwaka wa 2012, kimbunga cha Sandy na mazishi ya Nelson Mandela, Disemba mwaka 2013 .


Pia amewahoji viongozi wa Afrika kama vile rais wa zamani wa Tanzania, Jakaya Kikwete kama sehemu ya taarifa kuhusu biashara haramu ya wanyama pori pamoja na rais wa Uganda Yoweri Museveni. Mahojiano aliofanya na mgombea urais wa upinzani, Edward Lowassa mwaka 2015 yalizua gumzo sana katika vyombo vya habari nchini Tanzania na nje ya taifa hilo .


Miongoni mwa kazi za kipekee alizofanya BBC World Service ni pamoja na makala maalumu kuhusu meli ijulikanayo kama MV Liemba. Meli hiyo iliyoundwa na wajerumani wakati wa vita vya kwanza duniani ambayo bado inatumika huko Kigoma, Tanzania .


Mwaka 2019 aliweka historia nyingine kama mtangazaji wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kutangaza kipindi cha Focus on Africa TV na kuwa mtu wa kwanza kutangaza katika BBC World News akiwa amevaa hijab .


Wenzake wa BBC pia walimsifu Zuhura kwa mchango wake mkubwa wakati walipofanya naye kazi .


Mhariri wa Africa TV, Ian Booth kupitia ujumbe wa barua pepe wakati akitangaza kuondoka kwa mtangazaji huyo alisema- 'Zuhura tutakukumbuka sote na tunakutakia kila la kheri kwa siku zijazo'.


Mhariri wa BBC Swahili Caroline Karobia alimtaja kama 'Mwanahabari wa kipekee ambaye mahojiano yake na viongozi wa nchi mbali mbali, upinzani na wanaharakati yalikuwa ishara ya uanahabari wa kuigwa'.


'Tutakosa sana mchango wake na kufanya kazi naye, tabasamu lake lilimpa kila mtu uchangamfu' ameongeza Karobia .


Mtangazaji mwenzake Mariam Omar naye alikumbuka safari yake na Zuhura tangu walipokuwa katika Swahili redio. Mariam katika ujumbe wake ameandika;


'Nina historia nzuri na Zuhura tangu alipojiunga na Swahili Redio, nilipewa jukumu la kuwa mshauri wake, sijawahi kuwa na wakati mgumu naye - tumetoka mbali... ni historia ndefu'


Mwandishi mwingine wa BBC, Dinah Gahamanyi alimtaja Zuhura kama mtu mkarimu na mcheshi.


'Huwezi kukosa furaha ukifanya kazi na Zuhura na ilikuwa rahisi kushirikiana naye mkifanya kazi' ameongeza Gahamanyi

Post a Comment

0 Comments