Jeshi la DR Congo lafanikiwa kupambana na waasi wa M23

 


Ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limechukua tena udhibiti wa eneo la Jimbo la Kivu Kaskazini kutoka kwa waasi wa M23, moja ya makundi yenye silaha ambayo yanaendesha operesheni zao katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo yenye machafuko.


Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa iliripoti kwamba Vikosi vya Wanajeshi vya DR Congo vimechukua tena eneo la Kabaya, katika kundi la vijiji vya Kisigari, jana.


Iliongeza kuwa jeshi limewarudisha nyuma waasi wa M23, ambao walikuwa wakitishia kuizingira kambi ya kijeshi ya Rumangabo, ambayo hapo awali iliripotiwa kutekwa na waasi hao.


Mapigano yalizuka mapema wiki hii katika maeneo kadhaa huko Kivu Kaskazini, ambayo inapakana na Rwanda.


Kufuatia uvamizi huo wa waasi, Marekani ilitoa ushauri ikiwaonya raia wake dhidi ya kusafiri katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri wa madini.


Kundi la waasi la M23 - ambalo kimsingi ni la Watutsi wa Congo - lilianza tena mapigano mwaka huu, likiituhumu serikali ya DR Congo kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ya mwaka 2009 ambapo wapiganaji wake walipaswa kuunganishwa katika jeshi.


Wakati huo huo DR Congo inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 Tunasubiri majibu baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Christophe Lutundula Apala Pen'Apala jana kuishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23.


"Rwanda inasonga mbele...naweza kusema bila kusita, Rwanda imeshambulia kambi ya Rumangabo huko DR Congo...narudia tena M23 wakiungwa mkono na Rwanda walishambulia wanajeshi wa kimataifa wa Monusco [Misheni ya Umoja wa Mataifa nchini DR Congo]," Lutundula Pen'Apala alisema wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la AU huko Malabo, Equatorial Guinea, Mei 25.


Uhusiano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda ulikuwa umeanza kudorora baada ya Rais Felix Tshisekedi kuchukua madaraka mwaka wa 2019, lakini kuzuka upya kwa ghasia za M23 kumeongeza hali ya wasiwasi.

Post a Comment

0 Comments