Jeshi la Polisi lajitenga sakata la Mzee wa Yesu

 


Ikiwa imepita wiki moja tangu alipokamatwa na maofisa wa Idara ya Uhamiaji bila kujulikana alipohifadhiwa Askofu wa Kanisa la House of Prayer, Mulilege Kameka almaarufu kama Mzee wa Yesu, mkewe amesema hili ni tukio la tatu kwa mumewe huku Jeshi la Polisi likikana kujihusisha.


Mara zote tatu, mke wa askofu huyo, Greener Mwakabenga amesema mamlaka hiyo haijawahi kumpeleka mahakamani wala kuonyesha ushahidi au vielelezo vinavyobatilisha uraia wa mumewe.


Hata hivyo, juzi Mwananchi lilizungumza na Kamishna wa Uhamiaji, Dk Anna Mkakala aliyesema hana taarifa za kukamatwa kwa mtumishi huyo wa Mungu.


Alipopigiwa simu jana kuthibitisha iwapo amepata taarifa zozote kuhusu alipo askofu huyo, simu yake iliita bila majibu.


Hata alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Jumanne Murilo kama ana taarifa zozote juu ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kanisa alisema hahusiki na suala hilo kwani lipo nje ya mamlaka yake ya kiutendaji.


“Hatuhusiki nalo, hilo lipo chini ya Idara ya Uhamiaji. Wao ndio wana majibu yake,” alisema Kamanda Murilo.


Utata sasa wagubika kupotea Mzee wa Yesu

Hata hivyo, Msema wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mesele alisema analitambua suala hilo na wanalifanyia kazi.


Bila kueleza ni kitu gani hasa wanakifanya, alisema: “tutalishughulikia kuanzia kesho (leo).”


Jana gazeti hili lilienda kanisani kwa kiongozi huyo lililopo Boko Magengeni jijini Dar es Salaam na kukuta ibada ikiendelea katika kama kawaida huku waumini wakiiomba Serikali kulishughulikia suala hilo.


Akieleza mikasa ya kukamatwa kwa askofu huyo mara tatu kwa miaka tofauti, Greener alisema mara ya kwanza alikamatwa mwaka 2011 na watu waliojitambulisha kuwa wanatoka katika idara hiyo inayosimamia na kufuatilia masuala ya uraia.


“Baada ya kufuatilia ilibainika alipelekwa nchini (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) Kongo, lakini nako walimkataa kwa kuwa hakukuwa na nyaraka zozote zinazothibitisha kuwa ni raia wa nchi hiyo,” alisema Greener.


Baada ya Kongo kumkataa, alisema mumewe alirudishwa nchini na kupelekwa Kituo cha Polisi Tazara.


Kutokana na tuhuma za uraia wa mumewe, alisema alilazimika kwenda mahakamani kuthibitisha uraia wake, kesi ambayo walishinda.


“Nilikwenda mahakamani kufungua kesi...msingi wa kesi tulipewa hati ya mahakama kuthibitisha uraia wake na ushindi huo ni kwa sababu Serikali haikuwa na ushahidi wa tuhuma alizokuwa anapewa,” alisema.


Tukio la pili, alisema lilitokea mwaka 2019 walipovamiwa nyumbani kwao saa 10 alfajiri, mumewe akakamatwa kisha akapelekwa Idara ya Uhamiaji kwa mahojiano.Mwaka huo, alisema mumewe aliwekwa mahabusu kwa takriban miezi tisa bila kufunguliwa mashitaka na baada ya kufungua kesi ya kuomba kuachiwa kwake alisafirishwa kwenda nje ya nchi.


Hata hivyo, hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha tuhuma zilizokuwapo kuhusu utata unaodaiwa kuwapo kwenye uraia wa mumewe hivyo alirudishwa tena nchini.


“Mara ya tatu askofu alikamatwa Jumapili iliyopita tukiwa kanisani kwake, waliomkamata walidai ni watu wa Uhamiaji na walimchukua hadi leo hatujui alipo,” alisema mke wa mtumishi huyo. Kinachowashangaza alisema ni kwa nini anafuatwa kama jambazi bila kutumiwa wito kwenda kuripoti ofisi za idara hiyo muhimu.


Kuhani wa kanisa hilo, Nazer Nicholaus, alisema tangu watoe taarifa ya kukamatwa kwa kiongozi huyo bado mamlaka husika haijajibu chochote.


“Kama kweli si Mtanzania, kwa nini hawaonyeshi vielelezo, kwa nini hapelekwi mahakamani ili sheria ikachukue mkondo wake?” alihoji Kuhani Nicholaus.


Post a Comment

0 Comments