Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Nchi za Ulaya zatimiza masharti Rais Putin asizikatie gesi asilia


Mshirika 54 ya nishati barani Ulaya yametekeleza masharti ya Rais Vladimir Putin ya kufungua akaunti maalumu benki ili yaendelee kupokea gesi kutoka Russia.


Kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine tangu Februari 24, Umoja wa Ulaya (EU) ukishirikiana na Marekani uliiwekea vikwazo vya kiuchumi Russia ambayo nayo imejibu mapigo ambayo wababe hao wana lazima kuyatimiza masharti ya Rais Putin ili wasiikose nishati hiyo muhimu kwao.


Baada ya Russia kuondolewa kwenye mfumo wa malipo wa kibenki (Swift) halafu ndege zake kupigwa marufuku kuruka katika anga la Ulaya huku meli za mizigo nazo zikikata safari kwenda Russia, Taifa hilo halikunyamaza.


Kwa kutambua kwamba ndilo linalotoa asilimia 40 ya gesi asilia inayotumika viwandani hata kuzalisha umeme unaotumika katika mataifa yote ya Ulaya, lilizitaka nchi hizo kulipia kwa sarafu yake, ruble vinginevyo wataikosa bidhaa hiyo muhimu kwao.


Sharti hilo lilitolewa huku umoja huo nao ukifikiria kuachana na uagizaji wa gesi kutoka Russia, jambo linaloonekana kuwa gumu kwao, kwani hawana mbadala hivyo kulazimika kuinamisha kichwa kwa Putin anayeendeleza mashambulizi Ukraine inayosaidiwa na Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (Nato).


Katika masharti yake, mashirika ya nishati ya Ulaya yanatakiwa kufungua akaunti mbili Gazprombank, benki ya tatu kwa ukubwa nchini Russia. Akaunti ya kwanza yatazitumia kuweka sarafu ya Euro na ya pili itakuwa kwa ajili ya kuzibadili Euro hizo kwenda ruble ili kufanikisha malipo ya gesi kutoka Russia.


Sharti hili ambalo limeanza kutekelezwa na mataifa yasiyotaka kukatiwa gesi linawaumiza kichwa na kuwagawa viongozi wa Umoja wa Ulaya ambao tayari wamegawanyika kuhusu kutoagiza gesi kutoka Russia ili kuipunguzia uwezo wa kuendesha vita vinavyoendelea nchini Ukraine.


Viongozi hao pia wanafikiria namna ya kupunguza bei ya mafuta yanayonunuliwa Russia, kwani kupanda kwa bei yake kunaonekana kulinufaisha zaidi Taifa hilo hivyo kujiongezea nguvu za kuendelea kupambana na Ukraine, licha ya vikwazo lililowekewa.


Ukraine, Marekani na Canada zinaongoza kushawishi kupanga bei elekezi ya mafuta hayo au kuweka kodi itakayopunguza faida anayoipata Putin kwa kuuza bidhaa hiyo pamoja na gesi asilia na makaa ya mawe kusaidia kuendesha viwanda na uchumi wa Ulaya.


Ulipaji wa gesi na mafuta kwa Euro huku Russia ikipokea kwa ruble, wachambuzi wanasema ni namna ya kuonyesha kwamba Ulaya haitumii ruble wala Russia haipokei Euro, hali inayoonyesha vikwazo vilivyowekwa mwanzo bado vinaendelea kutumika.


“Hii ni biashara ambayo kila upande unajaribu kuficha sura yake,” alisema Profesa Alessandro Lanza, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha LUISS na mchumi mstaafu wa Shirika la Nishati Italia (Eni).


Shirika la mafuta na gesi asilia la nchini Australia nalo (OMV) lilisema: “Tunaahidi kulipa kwa wakati mara tu tukapopokea gesi kutoka Russia.”


Utata kwa watunga sera

Taifa lolote la Ulaya litakalogoma kulipa kwa mfumo unaopendekezwa kama ilivyojaribu kufanya Poland na Bulgaria basi hakutakuwa na kingine kutoka Gazprom, shirika la Taifa la gesi na mafuta la Russia zaidi ya kufunga bomba la bidhaa husika.


Mwezi uliopita nchi hizo mbili zilikataa kukubaliana na masharti ya Russia, kwa sasa hayapati gesi kutoka Russia. Wiki hii Finland nayo ilikatiwa huduma baada ya kuwasilisha maombi ya kujiunga Nato. Hofu iliyopo iwapo uamuzi huo utaendelea kutekelezwa basi bei ya nishati itapanda kwa kiasi cha kutoshikika kirahisi.


Viongozi hasa watunga sera katika mataifa ya Ulaya wanakosa msimamo kwa sasa juu ya lipi walichukue kutokana na hali inayoendelea kati ya kusimamia vikwazo vilivyowekwa kutofanya biashara na Russia au kinyume chake.


Wiki iliyopita, Eric Mamer, msemaji wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya alitahadharisha kwamba kufungua akaunti ya ruble kama inavyoagizwa na Russia ni kuvunjwa vikwazo ilivyowekewa Russia.


Na muda mfupi baadaye, Waziri wa Uchumi wa Umoja wa Ulaya, Paolo Gentiloni alisisitiza kwamba kufunga akaunti hiyo ni kinyume na vikwazo vilivyowekwa “jambo ambalo wengi hawalitekelezi.”


Baadhi ya maofisa nchini Italia wanaamini utaratibu uliowekwa hauvunji vikwazo vilivyowekwa kwani vinaihusu Benki Kuu ya Russia ambayo haihusiki kwa lolote kwenye ubadilishaji wa fedha hizo, kutoka Euro kwenda ruble hivyo kuliruhusu shirika lake, Eni kuendelea na utaratibu uliopo.


“Benki Kuu ndio imewekewa vikwazo sio sarafu ya ruble. Hata kama kampuni au shirika litalipa kwa ruble, litakuwa halijavunja vikwazo vilivyopo,” alisema ofisa wa Italia aliyezungumza na jarida la Washington Post la Marekani.


Shirika la Nishati Ujerumani (Uniper) lilisema limefungua akaunti katika Benki ya Gazprom “ili kukidhi vigezo vya kuendelea kupata gesi ila itaendelea kulipa kwa Euro.”


Naibu Waziri Mkuu wa Russia, Alexander Novak alisema mpaka wiki iliyopita, takriban nusu ya wateja wa nje wa Gazprom wamefungua akaunti za ruble.


Hata hivyo, wachumi wanaonya kwamba ingawa Russia inaonekana kupata faida nzuri kutokana kufanya biashara na Ulaya ila inaweza isinufaike sana kwa sababu imetengwa na mataifa mengi na kuondolewa kwenye mfumo wa malipo ya kimataifa.


Mchumi wa Chuo Kikuu cha Milan, Roberto Perotti alisema utaratibu uliowekwa unaonekana kuwa na manufaa ya kisiasa, kwani Russia ingeweza kukubali kupokea Euro kwa mafuta na gesi asilia inayouza Ulaya jambo ambalo lingezua kelele kutoka kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments