AU yataka uchunguzi ufanywe kufuatia mauaji ya wahamiaji katika mpaka wa Morocco na Uhispania

Umoja wa Afrika umetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka kuhusu vifo vya wahamiaji wasiopungua 23 waliofariki wiki jana Ijumaa.

Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema idadi ya vifo inaweza kuwa ya juu zaidi. Wahamiaji hao walikufa walipojaribu kuvuka hadi katika eneo la Afrika Kaskazini la Melilla, nchini Uhispania.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, alisema ameshtushwa na ana wasiwasi kuhusu jinsi wahamiaji wa Kiafrika wanavyotendewa walipojaribu kuvuka mipaka ya kimataifa.

Alizitaka nchi zote kuwatendea utu wahamiaji na kuacha kutumia nguvu kupita kiasi. Mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu, likiwemo Shirika la Kimataifa la Wahamiaji na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, yametaka uchunguzi ufanyike.

Mamlaka nchini Morocco ilisema baadhi ya waliofariki wameanguka kutoka juu ya ualinalotenganisha nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na Melilla. Zaidi ya watu 130 walifanikiwa kuruka ua hilo

Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alisema anajuta kwamba watu wengi walilazimika kufa walipokuwa wakitafuta maisha bora. Aliongeza kuwa wahalifu wanaofanya kazi kwenye mipaka ndio wa kulaumiwa kwa vifo vya wahamiaji.

Wahamiaji hao wanatarajiwa kuzikwa leo, lakini Chama cha Haki za Kibinadamu cha Morocco kimeonya dhidi ya kuwazika hadi vifo vyao vitakapochunguzwa.

 

Post a Comment

0 Comments