Fanya kazi mchana na usiku wananchi wapate maji - Mhandisi Sanga

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amemuagiza Mkandarasi anayejenga mradi wa maji wa Kibaoni katika Halmashauri ya Mpimbwe Mkoani Katavi kuongeza kasi na kufanya kazi mchana na usiku  ili kuwaondolea adha ya maji wananchi. 

Ametoa agizo hilo hivi karibuni alipotembelea Kata ya Kibaoni Wilayani Mlele kukagua utekelezwaji wa mradi.


Mradi wa Maji wa Kibaoni unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya Jemason Investment Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi 706,955,195.

Mhandisi Sanga alisema hatua iliyofikiwa kwenye mradi inawezekana wananchi wakaanza kunufaika na huduma ya maji na aliielekeza RUWASA Wilaya ya Mlele kumsimamia Mkandarasi ili kuhakikisha ifikapo tarehe 1 Julai, 2022 wananchi wawe wamefikishiwa huduma.

Aliongeza kuwa maelekezo ya Wizara siku zote ni kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na huduma hata kabla ya kumalizika kwa mradi.

"Mradi unapofikia tu hatua ya kutoa maji zoezi la kwanza liwe ni kuwafikishia huduma wananchi, msisubiri hadi shughuli zote za mradi zikamilike ndipo mfungulie maji, sio busara kuacha wananchi wanateseka wakati kwa hatua iliyofikiwa ya mradi inawezekana wao kupata huduma," alielekeza Mhandisi Sanga


Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Katibu Mkuu, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Gilbert Isaac alisema umelenga kunufaisha vitongoji vya Ndemanilwa, Kakuni, Ushirika na Isamvu na vitongoji vyote vya Kijiji cha Kibaoni.

Mhandisi Isaac alisema mradi unatekelezwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Alisema mradi huo wa upanuzi unatumia kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 22,000 kwa saa na kwamba walikuwa wakitumia matenki mawili ya lita 90,000 ambayo anasema yalisababisha upungufu wa huduma.

"Baada ya kupata fedha kupitia mpango huu wa maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 tunafanya upanuzi na maboresha ya miundombinu ili kunufaisha kijiji chote cha Kibaoni," alifafanua Mhandisi Isaac

Alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa tenki la ujazo wa lita 300,000 juu ya mnara wa mita 12 ikiwa ni tenki la zege, uchimbaji wa mitaro kilomita 11.2, ujenzi wa vituo 9 vya kuchotea maji Kibaoni, vituo 10 na chemba 32 katika Kijiji cha Inyonga.

 

Post a Comment

0 Comments