Mwanasiasa wa Kenya awaomba radhi Wasomali

Mgombea kiti cha Ugavana wa Nairobi kwa tikiti ya chama cha Jubilee, Polycarp Igathe Kamau, amelazimika kuomba msamaha kufuatia kauli yake iliyozua ghadhabu miongoni mwa wakazi wa Nairobi.

Igathe, ambaye amekuwa akishutumiwa kwa kulenga jamii fulani mahususi, alisema matamshi yake ni tofauti na kuelewa kwamba alikuwa akiwanyooshea vidole watu binafsi.

Akielezea matamshi yake ya awali, mwanasiasa huyo alisema alikuwa anazungumzia tu kutanguliza nafasi za kazi, uchumi na manufaa ya Nairobi.

Hatua ya Polycarp Igathe Kamau kuomba msamaha ilifuatia video iliyosambazwa sana mitandaoni kuhusu hotuba yake ya wiki iliyopita.

Katika kanda hiyo ya video alisema Bunge la Kaunti ya Nairobi, ambalo wanachama wake "wengi ni Wakikuyu, linadhibitiwa na wabunge watatu wa Kisomali, ambao wanazuiliwa mateka"

Hakuwataja majina Wasomali hao watatu alidai "wanadhibiti" Bunge la Wawakilishi la Nairobi.

"Kuna wajumbe 45 katika Bunge la Wawakilishi jijini Nairobi,wote wanatokea jamiii ya Wakikuyu,lakini kusema wote wanadhibitiwa na Wasomali watatu. Huo ndio ukweli. Kuzuiliwa mateka ndio neno halisi. Hata jana walikuwa wanafanya jambo ambalo sio halali," Igathe alionekana akisema.

Lakini sasa ametoa taarifa ya kuomba msamaha kwa kutoa kauli hiyo, akidai kuwa ilieleweka visivyo.

Matamshi ya awali ya mwanasiasa huyu yamewakasirisha sana Wasomali nchini Kenya.

Mbunge wa Garissa Aden Duale alikuwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri waliokosoa matamshi ya Igathe, akiyataja kama "kuwabagua Wasomali".


 

Post a Comment

0 Comments