Watoa huduma za afya wahimizwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa


Na Clavery Christian Muleba Kagera.

Naibu Katibu Mkuu (Afya), Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa OR-TAMISEMI Dr. Grace Magembe amewahimiza watoa huduma za afya kuwahudumia vizuri wagonjwa kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao, heshima na utu.

Amesema hayo katika ziara yake ya kukagua miundombinu ya Zahanati na Vituo vya Afya vilivyopokea fedha za miradi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 alipozungumza na watumishi wa Kituo cha Afya cha Kaigara kwa kuwasihi watoa huduma za afya kuwapokea, kuwajibu vizuri wagonjwa, kuwaelekeza kwa kuwatolea ufafanuzi mzuri kuhusiana na huduma zinazotolewa katika Vituo vya Afya na Zahanati.

"Watumishi wenzangu wa idara ya Afya, mgonjwa anapokuja kutibiwa, mjibu kwa kauli nzuri  lakini pia tuwe wepesi kutoa ufafanuzi kwa wagonjwa kuhusiana na  huduma zinazotolewa kwenye Vituo vya Afya na Zahanati,” amesema Dr. Magembe.

Dr Magembe ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la dharula katika kituo hicho na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha anasimamia na kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo ili liweze kumalizika haraka ndani ya muda unaotakiwa.

Pia ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya inayojengwa katika eneo la Marahara, kata ya Magata Karutanga na kuagiza kuwepo kwa mpango kazi ambao unaonesha kila hatua ya ujenzi pamoja na  kuimarishwa kwa kasi ya usimamizi na kuongeza kasi ya ujenzi. Pamoja na kukagua ujenzi wa jengo la mama na mtoto, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la upasuaji pamoja na nyumba ya watumishi katika Kituo cha  Afya Nshamba pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje  na jengo la maabara katika zahanati ya Buganguzi.  

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Evart Kagaruki  ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha ambazo zimeletwa wilayani Muleba kutekeleza miradi ya maendeleo na kumueleza Naibu Katibu Mkuu kuwa watahakikisha wanasimamia na kutekeleza kama alivyowaelekeza ili kazi iweze kumalizika kwa wakati.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Buganguzi Mhe. Renatus Theophili Rumota amesema kuwa ujenzi wa mradi ukikamilika utaweza kusaidia upatikanaji wa huduma za uhakika katika zahanati hiyo pamoja na kusaidia  kata za Kishanda, Ijumbi, Kabilizi na Ibuga ambazo baadhi ya vijiji vyake vinapata huduma ya afya katika zahanati hiyo ya Buganguzi.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Buganguzi Dr. Selina Sanga amemuomba Naibu Katibu Mkuu kuwaongezea watumishi katika Zahanati hiyo pale mradi utakapokamilika ili kuongeza nguvu kazi.


 

Post a Comment

0 Comments