Afisa Madini Mkazi wa
Mkoa wa Dodoma Mhandisi Nchagwa Marwa amewakaribisha wawekezaji wa madini
kuwekeza kwenye shughuli za uchimbaji wa madini kutokana na mkoa huo kuwa na
madini ya aina nyingi ikiwemo ya viwanda, ujenzi, vito na metali na kusisitiza
kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Mhandisi Marwa
ameyasema hayo leo Agosti 05, 2022 kwenye maonesho ya Nane Nane ya Kanda
ya Kati yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema kuwa
Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka mazingira rafiki ikiwa ni pamoja na
utoaji wa leseni za uchimbaji na biashara ya madini kwa wakati ili kuwezesha
shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kufanyika kwa tija.
Akizungumzia biashara
ya madini katika mkoa wa Dodoma, ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya
Madini imefungua masoko ya madini nchini na kusisitiza kuwa ofisi yake
imejipanga kutoa leseni za biashara na vibali kwa ajili ya
kusafirisha madini kwa haraka ikiwa ni mkakati wa kurahisisha shughuli za
biashara ya madini.
Katika hatua nyingine
amewataka wachimbaji wa madini kuzingatia matakwa ya Sheria ya
Madini ikiwemo kulipa ada za mwaka za leseni kwa wakati ili kuepuka kuchukuliwa
hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini na kufutiwa leseni hizo.
0 Comments