Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amefunga mafunzo ya siku tano ya
kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea
ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika
mafunzo hayo Mhe. Masanja amesema kuwa mafunzo hayo yametoa mbinu za
kuhakikisha hifadhi zinahifadhiwa vizuri ili kulinda wanyamapori na kuendeleza
utalii.
“Wataalamu wa masuala
ya uchunguzi wamejifunza mbinu za kuzuia uharibifu wowote unaoweza kutokea
kwenye maeneo ya hifadhi katika nchi wanachama wa Mkataba wa Lusaka (Lusaka
Agreement)”.
Amesema mafunzo hayo
yameshafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na Tanzania itaendelea
kushiriki kama nchi mwanachama ili kuzilinda hifadhi na wakati huohuo
kuendeleza utalii.
Naye, Mkurugenzi
Msaidizi wa Kuzuia Ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Robert Mande
amesema kuwa mafunzo hayo yataendelea kufanyika ili kutekeleza sera za Serikali
za kuendeleza uhifadhi.
“Lazima tuhakikishe
kuwa tunalinda rasilimali za wanyamapori ili watalii wanavyokuja waweze kuziona
na waweze kuwa na usalama”Mande amefafanua.
Ameongeza kuwa
washiriki zaidi ya 21 kutoka nchi wanachama wamejengewa uwezo katika masuala ya
uchunguzi, upelelezi, intelijensia na uendeshaji mashitaka ili waweze kufikia
viwango vya umahiri mkubwa kwa sababu makosa ya ujangili yanavuka mipaka ya
nchi na yanahitaji ushirikiano na vyombo vingine vya nje ya nchi.
Kwa upande wake
Mshiriki wa Mafunzo kutoka nchini Kenya, Bw. Jami Yamina amesema mafunzo hayo
yametoa mbinu mbalimbali za kutumia ili kuwakamata majangili na kuzikamata mali
zao na kuziwasilisha mahakamani.
“Tukiweza kuwakamata
hawa majangili tutakuwa tumefanikiwa kuzuia biashara hii haramu ya wanyamapori
” amesisitiza.
Mafunzo hayo
yamehudhuriwa na wataalamu wanachama wa Lusaka Agreement (unaojihusisha na
kuzuia uuzaji, usafirishaji wa wanyamapori pamoja na mimea) Grace Farm
Foundation, US Homeland Security na washiriki kutoka nchini Uganda, Kenya na
Tanzania.
0 Comments