https://monetag.com/?ref_id=TTIb Wafanyabiashara wa mbolea watakiwa kufuata taratibu | Muungwana BLOG

Wafanyabiashara wa mbolea watakiwa kufuata taratibu


Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya  Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Happiness Mbelle amewataka wafanyabiashara wa mbolea nchini Kufuata Sheria ya Mbolea Na. 9 ya 2009 na kanuni zake katika kufanya biashara hiyo.

Ametoa wito huo hivi karibuni alipotembelea na kukagua  duka  la mbolea la mbareaggrovet linalomilikiwa na Adam Mbare lililopo wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Happiness amewataka wauzaji wa maduka ya mbolea kuvaa vifaa kinga ( protective gear) wakati wote wanapokuwa dukani ili kujikinga na madhara yatakayotokana na kumwagikiwa na mbolea wakati akiendelea na majukumu yake.

Aidha, ameagiza wamiliki wote wa maduka ya mbolea kubandika vyeti vyao vya mafunzo pamoja na leseni ya mbolea inayomruhusu kufanya biashara hiyo.

Kwa upande wake muuzaji wa duka hilo (jina halikupatikana) alikiri kushiriki mafunzo ya mbolea na kutunukiwa cheti pamoja na kwamba hakuwa nacho dukani jambo ambalo halikubaliki kisheria.

Happiness ameendelea na ukaguzi katika maeneo mbalimbali mkoani Mbeya ambapo leo tarehe 6 Agosti, 2022 amefanya ukaguzi katika  Wilaya ya Rungwe, busekelo na Kyela mkoani Mbeya.

Pamoja na ukaguzi huo Happiness ameendelea kufatilia zoezi la usajili wa wakulima ili waweze kunufaika na  mbolea ya ruzuku itakayotolewa na Serikali kwa msimu wa kilimo wa Mwaka 2022/2023.

Post a Comment

0 Comments