Wajasiriamali waipa tano SIDO, walia na soko la bidhaa zao.

 


Na Ahmad Mmow, Lindi.

Baadhi ya wabanguaji wadogo wa korosho mkoani Lindi wamepongeza shirika la kuendeleza viwanda vidogo nchini(SIDO) Kwa kuwapa elimu na mashine za kubangulia korosho.


Wakizungumza na Muungwana Blogo jana kwa nyakati tofauti katika viwanja vya Ngongo manispaa ya Lindi ambako yanafanyika maonesho ya wakulima( Nane nane) kanda ya Kusini walisema SIDO ni mfano wa kuigwa kwa nia njema ya kuwaendeleza wajasiriamali katika mkoa wa Lindi.


Agia Mbinga wa kikundi cha wajasiriamali cha Juhudi kilichopo katika kijiji cha Liugulu wilaya ya Ruangwa alisema SIDO limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wajasiriamali wananyanyuka kupitia kazi zao.


Alisema SIDO licha ya kutoa elimu ya ujasiriamali kupitia mafunzo na semina lakini pia inatoa zana kwa vikundi. Akitoa mfano kikundi chao ambacho nicha kubangua korosho kimepewa mashine ya kubangulia.


" Kwajumla SIDO ndio wanasaidia na wametuwezesha kufika hapa tulipo. Wanatoa mafunzo kupitia hamashauri idara ya maendeleo ya jamii. Lakini pia wanatutembelea mara kwa mara," alisema Agia.


Mjasiriamali huyo alisema licha ya juhudi kubwa inayofanywa na SIDO lakini changamoto ipo kwenye soko. Kwani hawana soko la uhakika la bidhaa yao.


Alitoa wito kwa serikali kuwatafutia soko. Hasa kwa kuwajengea kituo kituo kimoja kama wauzaji wa madini walivyofanyiwa. 


" Soko la korosho lipo, tena zuri. Bali changamoto ni jinsi ya kufikisha sokoni. Wanunuzi wanataka mzigo mkubwa kuanzia walau tani saba ndio wanaweza kuja kununua tulipo. Sasa kama tungekuwa na kituo ingekuwa rahisi kupata mzigo mkubwa wanaotaka wanunuzi, tungekuwa kwenye eneo moja," alibainisha Agia.


Maelezo ya Agia yaliungwa mkono na Zuhura Nchila mbanguaji wa korosho katika kijiji cha Kilimani  hewa wilaya ya Nachingwea ambae pia alishukuru SIDO kwajitihada kubwa ya kutoa elimu na zana za kubangulia korosho.


Alibainisha kwamba shirika hilo linaweza kuwa mfano wa uwajibikaji kwa mashirika na taasisi za umma.


Lakini pia alisema changamoto kubwa ipo kwenye soko na mitaji kwa wajasiriamali. Nae pia alisema soko la korosho ni zuri lakini lipo mbali na gumu kufikiwa na wafanyabiashara wadogo.


Zuhura aliyetoa pongezi kwa Chama kikuu cha ushirika cha RUNALI kwa kuwa karibu na wajasiriamali ikiwamo kuwapeleka katika maonesho hayo na kubeba gharama zote alitoa wito kwa serikali kuwezesha mikopo na soko.


Kuhusu RUNALI alisema chama kikuu hicho kipo karibu na wakulima na wajasiriamali. Kwani yeye licha ya kupelekwa na chama hicho kwenye maonesho hayo lakini pia ndicho kilichompa vifungashio anavyotumia kufungia korosho anazouza.


Kaimu meneja wa SIDO mkoa wa Lindi, Isaack Daniel Kirigini alisema shirika hilo litaendelea kutoa elimu na vifaa kwa wajasiriamali. Kwani wajasiriamali wanachochea ukuaji wa uchumi wa nchi.


Alisema uchumi wa nchi  duniani kote umeshikwa na sekta binafsi. Na wajasiriamali ndio wanamchango mkubwa wa kuchochea uchumi.


 Alisema viwanda vidogo na wajasiriamali wanamchango mkubwa  wa kuzalisha bidhaa na kuongeza thamani ya mazao. Lakini pia aliweka wazi kwamba licha ya kutoa mafunzo na vifaa vya kazi lakini pia SIDO inakopesha fedha kwa wajasiriamali.


Post a Comment

0 Comments