Wizara ya Elimu yaandaa mkutano maalumu wa wadau kujadili mapitio ya sera

 


WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa mkutano wa wadau mbalimbali wa sekta ya elimu  ili kujadili mapitio ya sera na mafunzo ya mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala ya elimu nchini.

Hayo yamesemwa leo Septemba 25,2022  na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 Septemba 2022 Jijini Dodoma.

Waziri Mkenda amesema kuwa Mkutano huo unajumuisha, Wahadhiri, Waajiri, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za umma na Binafsi, Taasisi za Dini, Taasisi zinahusika na uendelezaji wa lugha, Wabunge, Wajumbe toka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Taasisi zisizo za Kiserikali, Jumuiya za kitaaluma, na Taasisi za Sayansi na Utafiti.

”Lengo la Mkutano huo ni kujadili Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mabadiliko ya Mitaa ya Elimu msingi ambapo timu ya Zanzibar inayopitia Sera na mitaala itaongozwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na wajumbe wengine kutoka Zanzibar”amesema Waziri Mkenda

Amesema kuwa majadiliano hayo yatatokana na hatua iliyofikiwa na mapitio hayo kupitia kamati maalumu zilizopewa majukumu hayo.

Aidha Waziri Mkenda amesema kuwa Serikali imezindua tuzo za waandishi bunifu zijulikanazo kama Tuzo za Mwalimu Nyerere, hivyo awakumbusha Waandishi Bunifu wa Riwaya na Mashairi kuwasilisha maandiko yao ili kuwania tuzo hizo.

”Mwisho wa kupokea Mawasilisho hayo ni Novemba 30, 2022 ambapo kwa taarifa zaidi kuhusu tuzo hizo na maulizo wanaweza kufuatilia katika akaunti maalumu za mitandao ya kijamii za tuzo Nyerere au mitandao na tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Elimu Tanzania-TET kwa anuani ya tuzonyerere@tie.go.tz”amesisitiza Prof.Mkenda

 

Post a Comment

0 Comments