Baada ya kuweka mikakati ya udhibiti kwa kutumia Akili Mnemba yaani Airtel Spam Alert na kuongeza elimu kwa wateja kwa lengo la kukataa Utapeli Mtandaoni , Airtel Tanzania sasa imefanikiwa kupunguza visa vya udanganyifu kwa asilimia 56 ndani ya kipindi cha robo mwaka ukilinganisha na kipindi kilichopita.
Mafanikio hayo yametokana na mkakati wa kiteknolojia wa hali ya juu wa uzinduzi wa huduma iitwayo Airtel Spam Alert – Kataa Matapeli, huduma ya kwanza barani Afrika inayotumia Akili Mnemba (AI) kutambua na kutahadharisha watumiaji wa mtandao huo kuhusu jumbe na simu za utapeli kwa wakati halisi, na hivyo kuwawezesha kuepuka vitendo vya kitapeli vya mara kwa mara kupitia simu ya mkononi.
Teknolojia hii bunifu ilizinduliwa kama sehemu ya kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya #SITAPELIKI inayoendeshwa kwa ushirikiano na serikali, huku Airtel Tanzania ikihakikisha vipaumbele vyake vya usalama kwa wateja vinaendana na juhudi za taifa katika kuleta usalama wa kidijitali.
Miezi michache tangu huduma hiyo izinduliwe, matokeo yameanza kuonekana. Hapo awali, Airtel ilikuwa inaongoza kwa visa vya utapeli vilivyoripotiwa—ikiwa na visa 5,187 mwezi Desemba 2024 na 5,876 mwezi Machi 2025, kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Lakini katika robo ya pili ya mwaka 2025, Airtel sasa inashika nafasi ya pili kutoka na mafanikio ya kupunguza utapeli, ikiwa nyuma kidogo ya TTCL iliyopunguza kwa asilimia 58.
“Hii si tu kuboresha teknolojia; ni uthibitisho kwamba tunawasikiliza wateja wetu na tunachukua hatua,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Beatrice wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo. “Tulitambua uzito wa tatizo hili na tukaleta suluhisho la kweli na linalotekelezeka. Kupungua kwa kasi kwa visa vya utapeli ni matokeo ya moja kwa moja ya juhudi hizi.”
Wakati Airtel inaendelea kupata mafanikio chanya, baadhi ya watoa huduma wengine wanakumbwa na ongezeko la visa hivyo. Ripoti hiyo hiyo ya TCRA inaonyesha kuwa Halotel ilishuhudia ongezeko la asilimia 67 ya visa vya utapeli katika robo ya pili ya mwaka, huku Vodacom nayo ikikumbwa na ongezeko la asilimia 34. Kwa upande wa Yas, kulikuwa na upungufu mdogo wa asilimia 0.2 tu.
Kwa ujumla, sekta ya mawasiliano, kwa mujibu wa TCRA, imeendelea kuwa tulivu katika robo ya pili ya mwaka 2025, huku kukiwa na ukuaji wa wastani katika mawasiliano ya simu, huduma za posta na usafirishaji wa vifurushi, pamoja na utangazaji. Hata hivyo, ni mwelekeo mpya wa Airtel kutoka kuwa katika hatari hadi kuwa mstari wa mbele katika tahadhari unaojitokeza kwa nguvu zaidi.
“Kwa kutumia zana za kisasa za AI na kwa kushirikiana kwa ukaribu na wadhibiti pamoja na kampeni zinazolenga kuelimisha jamii, tumeonyesha kuwa hata changamoto kubwa zinaweza kugeuzwa kuwa fursa. Na hii ni mwanzo tu,” alisema Mkurugenzi wa mawasilaino Bi Betrice Singano alipozungumza na gazeti letu.
0 Comments