F Mwenge waweka jiwe la msingi chujio la maji Jorodom | Muungwana BLOG

Mwenge waweka jiwe la msingi chujio la maji Jorodom

Na John Walter -Hanang’, Manyara  Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndugu Ismail Ali Ussi, amekagua na kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Chujio la Maji Jorodom–Katesh, mradi mkubwa unaotekelezwa kwa lengo la kurejesha huduma ya majisafi katika mji wa Katesh, kufuatia maafa ya maporomoko ya Mlima Hanang’ yaliyotokea Desemba 3, 2023.

Akizungumza akiwa eneo la mradi, kiongozi huyo alitoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huu muhimu kwa afya na maendeleo ya wananchi.

Ussi alisisitiza kuwa maji safi ni msingi wa maisha bora na maendeleo endelevu hivyo BAWASA wanastahili pongezi kwa usimamizi mzuri.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya maji na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Mhandisi Rashid Cherehani alisema kuwa ujenzi wa chujio hilo utagharimu kiasi cha Shilingi 1,154,320,346.90 hadi kukamilika kwake. 

Alieleza kuwa mradi huu ulianzishwa baada ya maafa makubwa kusababisha uharibifu wa miundombinu ya maji, na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa maelfu ya wakazi wa Katesh.

Mradi huu umetayarishwa na kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA), na ni sehemu ya juhudi za dharura za Serikali kurejesha huduma muhimu kwa wananchi. Utekelezaji wake ulianza rasmi tarehe 18 Septemba 2024 na unatarajiwa kukamilika ifikapo 30 Julai 2025.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa BAWASA, Mhandisi Iddy Msuya, kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na:

Ujenzi wa kidakia maji chenye uwezo wa kuzalisha lita 2,500,000 kwa siku, Ujenzi wa miundombinu ya kuchuja na kutibu maji kwa ubora wa kimataifa.

Mhandisi Msuya alibainisha kuwa hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 98, na utakapoanza rasmi kufanya kazi, utanufaisha zaidi ya wananchi 35,513 kutoka kata za Ganana, Jorodom, Katesh, na Dumbeta.   

Mradi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama kwa saa 24, kupunguza hatari ya magonjwa ya milipuko, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mji wa Katesh.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Almishi Issa Hazal, alisema kuwa hali ya upatikanaji wa maji wilayani humo inaendelea kuimarika kwa kasi kutokana na miradi madhubuti kama huo. 


Post a Comment

0 Comments