https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mbinu zitakazokusaidia kutimiza malengo yako | Muungwana BLOG

Mbinu zitakazokusaidia kutimiza malengo yako


Kila mwanzo wa mwaka tunakuwa na malengo mengi na mipango ya kuboresha afya zetu. Ni katika kipidi kama hiki ambapo wengi tuna kasumba ya kupanga kupunguza uzito, kuboresha afya, kuongeza bidii kazini, kuboresha ujuzi, na mengineyo mengi.

Miezi miwili mitatu mbeleni hizi habari zote tunasahau. Afya inageuka kitendawili, malengo yanapotea na tunarudi kwenye kasumba za mwaka jana na malengo hubaki kiporo hadi mwakani.

Je hivi ndivyo tunavyopenda tuishi? La hasha. Haya siyo maisha, ni vizuri basi kuangalia jinsi ya kuweza kujiweka sawa kwenye malengo yako ili uweze kutimiza mambo machache sana yenye faida kubwa kwa maisha yako yote.

Fahamu kuwa, kubadilisha tabia siyo swala rahisi. Ingekuwa rahisi kila mtu angekuwa anafanikiwa maishani na kushinda vikwazo na majaribu. Kufanikiwa ni swala linalohitaji uamuzi mgumu na wenye malengo makubwa ya muda mrefu. Ukiwa mtu wa kufata mkumbo huwezi kutimiza malengo, sababu huoni umuhimu wa kubadilisha tabia, maana hutakuwa na nia ya dhati.

Wengi wetu huacha juhudi za kupunguza mwili, kuboresha lishe, kufanya mazoezi na mengine mengi sababu walikuwa wanafata mkumbo. Hawakuwa na nia ya dhati ya kutimiza malengo. Hii siyo njia bora ya kufanya maamuzi yako maishani.

Wengi wetu tuko hodari kufanya juhudi kazini ili kuboresha kazi zetu, lakini linapokuja swala la maisha binafsi huwa hatuelewi cha kufanya. Pengine hii hutokana na ukweli kuwa wengi tumezoea kuamuliwa mambo na kufanya maamuzi, hasa binafsi inakuwa ni swala gumu kidogo na lisilowezekana bila kushurutishwa.

Kama unawaza hivyo inabidi ufahamu kuwa, mafanikio yako mwaka huu, na miaka mingine ijayo, yanategemea leo utaamua kuchukua uamuzi gani mgumu juu ya maisha yako. Leo ndio siku ya kwanza kwa maamuzi magumu yatakayobadilisha maisha yako.

Jinsi ya kufikia malengo
Je unawezaje kufikia malengo yatakayokupa moyo kufanya mambo makubwa zaidi ? Hapa tunaweka  vipengele vikuu 4 vinavyoweza kukupa mawazo ya kuweza kufikia malengo yako.

Chagua vitu muhimu
Wote tuna malengo mengi ya kufikia. Ila kumbuka vichache na muhimu ni bora kuliko vingi visivyoweza kufikika. Usiwe mtu wa kupanga malengo mengi yasiyo na msingi. Ukiona una malengo mia wakati mwaka jana hukuweza kutimiza hata moja jua kuwa umekurupuka tu.

Chagua malengo machache na yenye umuhimu mkubwa na uzito kwa maisha yako. Hakikisha kuwa una nia ya dhati kuyatimiza. Bila nia kwenye malengo yako utakuwa unacheza mchezo wa pata potea, na hapa utakuwa umeshindwa kabla hujaanza mbio zako.

Kumbuka, kila mmoja anapenda kufanikiwa, ila siyo kila mtu anaweza kufanya jitihada za kufanikisha malengo yake. Hivyo, angalia kile kinachowezekana na ulicho na nia nacho zaidi.

Chagua malengo yanayofikika
Je una uwezo wa kufikia malengo yako? Je una nia ya dhati kutimiza malengo yako?

Hakikisha malengo yako yawe yenye kuweza kufikika siyo kusadikia. Sina maana ya kukuvunja moyo, lakini nashauri ufanya vile vinavyowezekana kwa sasa, ukishapata mafanikio kwa vitu vidogo, vile vikubwa vitawezekana pia. Ni kama unapanga ngazi, huwezi kupanda mlima kilimanjaro wakati hata kutembea kilomita mbili kwa mguu ni kazi ngumu sana kwako. Hapo utakuwa unabomoa balada ya kujenga.

Cha muhimu ni kuwa, usijiharibie nafasi ya kufanya vitu muhimu na kufanikiwa kwa kuweka malengo yasiyofikika na ukaishia kukata tamaa. Malengo ni hatua, anza na yale yanayowezekana kwa sasa, mengine utayaweza tu baada ya kupata mafanikio.

Panga muda wa kufikia malengo
Ukiwa na nia, ipo siku malengo yako yatatimia. Je unataka iwe baada ya muda gani?

Ili kuweza kutimiza malengo yako, ni vizuri kupanga muda maalumu wa kutimiza malengo yako. Kupanga muda muafaka hukusaidia kujua nini cha kufanya na wakati gani ili kuweza kufanikisha kile ukitakacho. Anza na yale malengo yaliyo na uharaka na umuhimu zaidi. Kama malengo yako hayana haraka weka yawe baadae na fanya vile vitu muhimu kwanza. Huna haya ya kufanya kitu kisicho cha lazima leo wakati kuna viporo vingi vinavyohitaji muda wako wa haraka.

Fanya jambo kila siku
Tabia ni mazoea. Mazoea haya huweza kujengwa kwa kufanya kitu kila siku. Wengi wetu tunaweza kufanya mambo tunayoyapenda kila siku bila kukoma. Lakini si kila jambo tunalopenda kufanya huwa linatuletea maendeleo maishani. Kupiga uvivu au kuendekeza starehe ni vitu rahisi kufanya maana havitumii nguvu wala nguvu ya ubongo, lakini ikifika saa ya kufanya kazi muhimu huwa ni shuluba na mwishowe kuishia kuahirisha hadi kesho. Na hii tabia hujirudia, hadi uzeeni.

Lakini, unafahamu kuwa ufanisi ni tabia na unaweza kujifunza na ukiizoea itakuwa rahisi kufanya zaidi kuzembea? Ili kuwa na ufanisi katika kufikia malengo yako, panga ratiba ya kufanya kitu kidogo kila siku kinachohusiana na kutimiza lengo lako kubwa. Hii itakufanya ujenge kasumba ya uwajibikaji.

Kubadilisha tabia si kitu rahisi, hivyo ni vizuri kufahamu kuwa unaweza kubadilisha tabia kwa kufanya jambo unalopenda kila siku. Kila mtu anapenda kufikia malengo, lakini swala linalotuangusha sana ni uvivu. Lakini unafahamu kuwa unaPanga ratiba ya kufanya jambo moja kila siku ili kuweza kufikia malengo yako. Hakikisha kuwa hulali bila kufanya kitu.

Maisha ni mipango. Kila mwaka tunaweza kujipima kwa kile tulichokiongeza au kukipoteza. Kumbuka kuwa kila kitu kiko kwenye uwezo wako na wewe una maamuzi yote. Ili uweze kufanikiwa, panga malengo machache, andika kwenye karatasi, na kisha jaribu kuyatimiza kabla ya kuanza kuwaza malengo makubwa zaidi. Maisha hayana haraka, ila huenda kwa hatua ambazo haziwezi kuepukika kama unahitaji maendeleo yaliyo imara na ya muda mrefu.