UN yakosoa athari mbaya za misimamo hasi ya Trump kwa uhuru wa vyombo vya habari


Tangu alipochukua hatamu za kuiongoza Marekani tarehe 20 Januari mwaka 2017, Rais Donald Trump amekua akielekeza panga lake kali kwenye vyombo vya habari vinavyokosoa utendaji na mienendo yake.
Trump anaamini kuwa, vyombo vya habari vinasema uongo na wadau wa vyombo hivyo ndio watu wanaosifika kwa kughushi zaidi duniani; kwa sababu hiyo daima amekuwa akiwashambulia kwa maneno makali. Mwenendo huo wa rais wa Marekani umekosolewa na Umoja wa Mataifa.
Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika kulinda uhuru wa kusema na kujieleza, David Kaye Jana Jumanne aliashiria mashambulizi makali ya Ikulu ya Rais wa Marekani, White House dhidi ya vyombo vya habari na kukosoa athari mbaya za mienendo hiyo ya Trump kwa uhuru wa vyombo vya habari. Kaye amesema anatajia kwamba, hujuma na mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari yatapungua kwa kuondoka Donald Trump katika White House. Ripota huyo wa Umoja wa Mataifa amesema: Katika kipindi cha miaka minne iliyopita Trump ametumia mbinu iliyokwaza na kutatiza uhuru wa vyombo vya habari. Kaye ameongeza kuwa vitendo vya Donald Trump vya kuwashambulia waandishi wa habari na kueneza uongo dhidi yao ni kielelezo cha kuhujumu waandishi na vyombo vyao vya habari. Amesisitiza kuwa mwenendo huo wa Trump umekuwa na taathira hasi kwa uhuru wa vyombo vya habari kote duniani.



Ukosoaji wa wazi wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mienendo ya Rais Donald Trump wa Marekani na namna kiongozi huyo anavyoamiliana na vyombo vya habari unafichua sehemu ndogo ya picha halisi ya madai yanayotolewa na nchi za Magharibi kuhusiana na uhuru wa kusema na kujieleza. Trump, akiwa Rais wa nchi inayodai kuwa kinara wa uhuru duniani, anaamini na kukubali uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari vinavyomsifu yeye, kumtukuza na kusifia siasa na hatua zake, na hawezi kustahamili ukosoaji wa aina yoyote dhidi ya utendaji, sera na siasa zake. Donald Trump amekuwa akivishambulia vyombo vya habari vinavyoikosoa serikali yake akiviita kuwa ni "feki" na kwamba vinaeneza "habari za uongo". Ukurasa wa Twitter wa kiongozi huyo umejaa hujuma na mashambulizi makali dhidi ya vyombo vya habari na waandishi wa habari wanaokosoa na kuchambua utendaji wa serikali yake.
Gubu na mzimu wa Trump dhidi ya vyombo vya habari ulikuja juu zaidi baada ya kufichuliwa habari za ndani za maisha yaliyojaa ufuska na utovu wa maadili ya kiongozi huyo na kuanika sera zake zilizofeli katika siasa za nje. Donald Trump hakutosheka na kuwahujumu waandishi habari mitandaoni bali amekuwa hata akiwashambulia waziwazi na ana kwa ana katika vikao na mikutano ya wazi.
Tunapotazama kesi mbalimbali za hujuma za Donald Trump dhidi ya vyombo vya habari tunaona kuwa, kiongozi huyo wa Marekani amekuwa akitumia mbinu yake ya siku zote yaani kutoa vitisho na mashinikizo makubwa kwa ajili ya kuwatia woga waandishi wa habari na kutaka kuwalazimisha wakubaliane na matakwa na mitazamo yake ya kijuba na kibeberu. Hata ahivyo mbinu hiyo haikufua dafu na badala yake vyombo vya habari vya Marekani na kwengineko vimezidi kumuandama na kukosoa sera na utendaji wake. Kwa mfano tu mwezi Agosti mwaka 2018 karibu magazeti na majarida 350 ya Marekani yalichukua hatua ya pamoja na kuchapisha makala iliyokosoa mwenendo wa Trump wa kushambulia na kuhujumu vyombo vya habari.