Zitto, Lissu wazungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar


Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu wamezungumzia barua ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).


Wote wawili walisema suala la makubaliano halitakuwa kitu cha kwanza kufanyika, ingawa, kwa mujibu wa Zito, suala hilo linajadiliwa katika ziara ya mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad kutembelea waathirika wa matukio ya uchaguzi.


Kauli ya Zitto imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Mwinyi aeleze kuwa aliiandikia ACT-Wazalendo kuomba jina la Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kuwa Katiba inaelekeza nafasi hiyo iende kwa chama kilichopata zaidi ya asilimia kumi za kura, na kwamba katika baraza lake la mawaziri 14, hakuteua wawili kwa sababu ametenga nafasi hizo kwa ajili ya wawakilishi kutoka ACT-Wazalendo.


Akizungumza jana katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika kwa njia ya mitandao ya Zoom na Youtube, Zitto alisema hawakujibu barua ya Dk Mwinyi kutokana na msimamo wao wa kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 na 28.


“Sisi tunaona hakukuwa na uchaguzi Zanzibar na hii imeshaelezwa na mwenyekiti na mimi,” alisema Zitto akirejea msimamo wa Maalim Seif Sharif Hamad aliyegombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.


Alipoulizwa sababu za kupokea barua ya Dk Mwinyi wakati hawatambui matokeo ya uchaguzi, Zitto alisema “kwa nini tusipokee wakati imeletwa na imepokelewa?''


“Hatukupeleka jina kwa sababu hatukuukubali huo uchaguzi. Kama chama tuna michakato ya demokrasia. Uamuzi umeshapitishwa kwamba hatuutambui huo uchaguzi,” alisema.


Hata hivyo, alisema taarifa rasmi ya chama hicho haijatolewa kwa sababu bado Maalim Seif anafanya ziara za kutembelea waathirika wa matukio ya uchaguzi na kufanya vikao vya mashauriano.


“Zanzibar ina historia ya kugombea uchaguzi na kukubaliana,” alisema.


“Tunakumbuka mwaka 1999 kulikuwa na mwafaka uliosimamiwa na Emeka Anyaoku aliyekuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola.”


Alitaja pia mwafaka wa pili wa mwaka 2001 na mazungumzo ya mwaka 2009 kati ya Rais Amani Karume ulioanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa.


“Kwa hiyo kuna mifano ya makubaliano, iwe ni kwa mwafaka au makubaliano. Tumewaambia wanachama wetu kwamba tunafanya vikao vya ndani. Kwa sasa siwezi kusema tutashiriki au hatutashiriki. Kwa sababu hiyo inategemea michakato ndani ya chama,” alisema.


Kauli ya Zitto iliungwa mkono na Lissu anayeishi Ubeligiji aliyesema kuna uwezekano kifalsafa kwa ACT-Wazalendo inayopinga matokeo ya uchaguzi, kukubali wito na kufanya mwafaka.


“Kukubaliana si kushindwa. Makubaliano si kitu kigeni,” alisema.


“Nelsona Madela, Oliver Thambo na chama cha ANC hata baada ya mapambano mengi walikaa na kufanya makubaoani na wakandamizaji wao,” alisema, akimaanisha mazungumzo na serikali ya Afrika Kusini yaliyomaliza siasa za kibaguzi mwanzoni mwa miaka ya tisini.


Lissu na mustakabali wa upinzani

Katika mkutano huo, Lissu pia alieleza mkakati wa vyama vya upinzani vya Chadema na ACT Wazalendo, akisema vitaendelea kuilinda imani ya wananchi waliojitokeza kuwaunga mkono wakati wa kampeni.


“Wananchi walisimama nasi kwa kuamini kaulimbiu yetu ya kuwapa uhuru,” alisema Lissu.


“Walitukaribisha na kujadiliana nao. Walituchangia rasilimali zao, ikiwemo fedha. Kwa kuwa wananchi walikuwa nyuma yetu, nguvu yao haiwezi kupotea hivi hivi.”.


Huku akiwaonya wanachama wa chama hicho kuwa wakati ujao utakuwa mgumu zaidi, alisema bado wanaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.


“Hatuko peke yetu katika vita hii, tuna wenzetu katika eneo la maziwa makuu, bara la Afrika na jumuiya ya kimataifa. Tuna huruma ya dunia,” alisema.


Alirejea majadiliano ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya yaliyojadili Tanzania wiki iliyopita akisema “huo ni mwanzo tu”.


Alitaja hatua nyingine za kimataifa kuwa pamoja na kupeleka malalamiko kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) na kwa nchi wahisani.


“Tunataka kuwaambia waliotenda makosa haya kuwa hawana pa kujificha. Makosa haya lazima yawekwe wazi na yachukuliwe hatua,” alisema.


Lissu, aliyeondoka nchini Novemba 10 baada ya kudai kutishiwa usalama wake, alisema ataendeleza mapambano yake akiwa nje ya nchi kama chama tawala cha Afrika Kusini ANC kilivyopambana na serikali ya makaburu.


Alisema viongozi wa ANC--Oliver Tambo, Thabo Mbeki na wengineo-- walikuwa nje ya nchi wakati wakiendelea na mapambano kwa hiyo kuwa nje hakumzuii kupambana.


Kuhusu kurejea nchini, Lissu alisema anataka kwanza afutiwe makosa yote dhidi yake na pili serikali iwatajie wananchi watu waliomshambulia kwa risasi 16.


Kuhusu kuitaarifu polisi kuhusu tishio la usalama wake, Lissu alisema chombo hicho hakikuchukua hatua alipotaarifu tishio kama hilo mara ya kwanza.

Post a Comment

0 Comments