Afariki dunia baada ya kunywa dawa ya kusafisha nyota

 


Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamsaka mtuhumiwa Dela Megejuwa Lwaho (44) kwa kusababisha kifo cha mtoto wake Juma Dela Megejuwa (12) na watu wengine wawili kuzirai baada ya kuwapa dawa ya miti shamba idhaniwayo kuwa na sumu ili wasafishe nyota zao. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Januari 18,2021 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Januari 16,2021 majira ya saa tisa na nusu alasiri katika kijiji cha Mwaningi kata ya Bulige wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga. 

Marehemu pamoja na wenzake wawili waliotambulika kwa majina ya Loya Nsalala Ngusa (66) ambaye ni jirani wa mtuhumiwa na Bahati Ludahila Ngusa (25) mkazi wa Shilima Kwimba mkoani Mwanza ambaye ni mgeni aliyefikia nyumbani kwa mtuhumiwa, walipewa dawa hiyo na Mganga wa jadi, Juma Dela Megejua (44) ambaye ni baba wa mtoto aliyefariki ili wasafishe nyota zao

ACP Debora Magiligimba amesema mtuhumiwa (mganga wa jadi) alikimbia mara baada ya tukio hilo na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Halmashauri Mji Kahama kwa uchunguzi zaidi, na wenzake wawili wapo kituo cha afya Chela kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri

Pia, ametoa wito kwa waganga wa jadi kuwa na uhakika na matumizi ya dawa zao pamoja na matumizi mazuri ya vibali/leseni zao ili kuepuka kusababisha vifo na madhara kwa wateja wao

Post a Comment

0 Comments