Halmashauri ya wilaya ya Masasi yatoa mafunzo kwa Wenyeviti wa vijiji 166

 


WENYEVITI wa vijiji 166 kutoka  kata 34 za halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara   wamepatiwa mafunzo maalumu yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kutekeleza wajibu na majukumu yao. 

      Aidha,mafunzo hayo ya siku moja yanalenga kuwapa ufahamu wenyeviti hao kutambua vema namna ya kuzingatia hasa katika kupokea na kujadili taarifa za makusanyo ya fedha za ushuru, ada na mapato mengine yanayopaswa kukusanywa ndani ya kijiji kwa mujibu wa sheria zilizopo.

     Mafunzo hayo yametolewa na menejimenti ya halmashauri ya wilaya ya Masasi chini ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Changwa Mkwazu ambapo yalifanyika katika ukumbi wa zamani wa mikutano wa halmashauri hiyo mjini Masasi.

      Akizungumza katika mafunzo hayo kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Lyoba Magabe alisema kuwa halmashauri ya wilaya ya Masasi imeamua kutoa mafunzo hayo kwa wenyeviti wa vijiji ili kuwajengea uwezo wenyeviti hao waweze kutekeleza kazi zao kwa ufanisi zaidi kwenye maeneo yao pindi wanapotoa huduma kwa wananchi.

      Alisema kuwa wenyeviti hao wapo ambao wengi wao ni wapya katika nafasi hizo hivyo wakipata mafunzo hayo yatawasaidia kufahamu vema majukumu yao pia mipaka ya kazi wanazozifanya kwenye maeneo yao na kuepeka kuiingiliana majukumu na watendaji wa kata na kufanya shughuli za kiserikali kufanyika kwa ufanisi.

      Magabe alisema baadhi ya mambo ya msingi ambayo wenyeviti hao wanapaswa kuyafahamu ni pamoja na muundo wa serikali ya kijiji, wajibu na majukumu ya mkutano mkuu wa kijiji, muundo wa halmashauri ya kijiji, majukumu ya halmashauri ya kijiji na muundo wa kamati za halmashauri ya kijiji.

       Awali akifungua mafunzo hayo mwenyekiti wa halmashauri hiyo ya wilaya, Ibrahimu Chiputula alisema kuwa uamuzi huo kwa halmashauri wa kutoa mafunzo kwa wenyeviti hao utaleta tija.

      Chiputula alisema serikali ya kijiji huundwa katika kijiji kilichoandikishwa kwa mujibu wa kifungu na 22 cha sheria na 7 ya sheria za serikali za mitaa.

     "Nampongeza sana mkurugenzi kwa jambo hili kwani itapunguza malalamiko lakini pia mivutano kati ya watendaji wa kata na nyinyi wenyeviti hivyo mafunzo hayo ni muhimu kwenu," alisema Chiputula

      Victoria Mpande mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha. alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuwapa muongozo katika kutekeleza majukumu yao.

       Alisema hivyo anaiopongeza halmashauri kwa kuamua kutoa mafunzo hayo kwa wenyeviti hao wa serikali za vijiji.

Post a Comment

0 Comments