Jan 23, 2021

Waziri Jafo azitaka Halmashauri ambazo hazikuwalipa fedha za kujikimu walimu ajira mpya kulipa ndani ya wiki moja


Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo ametoa wiki moja kwa halmashauri zote ambazo zilipokea walimu wa shule za Sekondari za ufundi na hazijawalipa fedha za kujikimu kuhakikisha zinawalipa fedha hizo kwa walimu hao.

Waziri Jafo ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na wakuu wa mikoa yenye shule hizo na wataalamu kutoka mikoa 9, Mkutano uliofanyika kwa njia ya Mtandao (Video Conference) juu ya uboreshaji wa shule hizo ambazo miundombinu ilikuwa chakavu ziliboreshwa kwa sh. Bilioni 16.4 .

Amesema kuna baadhi ya halmashauri hazijafanikisha kuwalipa walimu wapya fedha za kujikimu na kusababisha walimu hao kufanya kazi katika mazingira magumu sana.

"Natoa wiki moja kwa Halmashauri ambazo hazijawapa fedha za kujikimu walimu ambao tumewapangia kufundisha katika shule hizo  staki kuwaona walimu wanafanya kazi wakiwa na msongo wa mawazo ‘Stress’ muwalipe haraka ". amesema Waziri Jafo.

Waziri Jafo pia amewaagiza wakuu wa mikoa 9 yenye shule za ufundi za sekondari za serikali kuhakikisha wanakuwa walezi wa shule hizo ili zitoe vijana wenye umahiri wa kutosha na wabobezi kwenye vitu mbalimbali.

Waziri Jafo amebainisha kuwa wakuu hao wa mikoa wenye shule hizo waweke utaratibu wakuzitembelea shule ikiwa ni pamoja na  kuongea na waajiriwa wapya ili kueleza kwa mapana juu ya mikakati ya serikali ya kuinua ubora wa shule hizo.

“Nawaagiza wakuu  wa mikoa 9 yenye shule za ufundi za sekondari za serikali kuhakikisha wanakuwa walezi wa shule hizo, maafisa elimu wa mikoa na Halmashauri husika hakikisheni mnafuatilia maendeleo ya ufundishaji  na ujifunzaji katika shule hizo,” amesema.

Amesema uimaishwaji wa shule hizo ni baada ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutoa dira ya kuelekea uchumi wa viwanda, na  mwaka 2016 wakaona ni vyema wakaanza kutoa wataalamu tangu ngazi za chini kabisa.   

Amesema maandalizi hayo ya  wataalamu hao watakaotoka katika shule hizo za sekondari za ufundi ambapo hatua zimechukuliwa ili kuimarisha utoaji wa elimu ya ufundi na kuifanya iendane na mahitaji na ushindani katika soko la ajira.

Amebainisha kuwa tangu mwaka 2015 hadi 2020 Serikali  imetoa  jumla ya sh. Bilioni 16.4 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule hizo yakiwemo vyumba vya madarasa, Ofisi, matundu ya vyoo na karakana za ufundi katika shule hizo.

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho imepeleka walimu kwa uwioano wa  Bwiru (walimu 16), Chato(walimu 18), Ifunda(walimu 16), Iyunga(walimu 17), Moshi (walimu 17), Mtwara(walimu 15), Musoma(walimu 16), Mwadui(walimu 18) na Tanga( walimu 17).

Amesema katika kiziimarisha shule hizo ziweze kuleta mabadiliko chanya  jumla ya sh milioni 30 zimetengwa kwa Kila shule kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia na vifaa vya mafunzo.

Waziri Jafo amesema maboresho yaliyofanyika katika shule hizo ni makubwa huku akiwataka wakurugenzi watendaji wa Halmshauri na wasimamizi wa shule hizo  kuhakikisha miundombinu na vifaa vinatunzwa.

“Na pale inapotokea ubovu au uchakavu wa miundombinu na vifaa vyake, Halmshauri haina budi kufanya matengenezo kupitia mapato yake ya ndani,” amesema.

Aidha amebainisha kuwa mbali na uwekezaji wa fedha hizo, Serikali pia imeajiri walimu 150 ambao wamegawanywa katika shule zote tisa lengo likiwa nikuziwezesha kupatikana kwa tija iliyokusudiwa ya kuwafanya Watoto wa kitanzania kuwa na ujuzi na maarifa yakuweza kujiajiri.

Ameongeza kuwa “hatutegemei kuona, wanafunzi wakiwa shuleni wanajifunza nadharia pekee yake, tunataka  wajifunze pia kwa vitendo ili wawe na ujuzi wakuzalisha baadhi ya vitu wanavyo jifunzia kama chaki, Vijiti vya kusafisha kinywa (toothpick)” amesema.

 

KWA HABARI ZAIDI <DOWNLOAD HAPA>
Share:
Loading...

Popular Posts

Copyright © MUUNGWANA BLOG | Powered by Blogger