https://monetag.com/?ref_id=TTIb Halmashauri zitumie fedha kwa utaratibu- Mabula | Muungwana BLOG

Halmashauri zitumie fedha kwa utaratibu- Mabula


Niabu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ameibana Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kurejesha fedha kiasi cha shilingi milioni 418 ilizopewa na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja katika manispaa hiyo.


Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Iringa katika kikao kazi  Dkt Mabula alisema fedha ilizopewa Manispaa ya Iringa ni mkopo kwa ajili ya kupima viwanja na siyo kwa ajili ya shughuli nyingine za halmashauri.


"Wizara imetoa fedha ili upime viwanja na kuuza na baadaye urudishe fedha lakini ninyi badala ya kurudisha fedha mmetumia kwenye mambo mengine, wenzenu Geita faida waliyopata katika mradi kama huu walinunua gari la idara ya ardhi, hatuwezi kutumia fedha kwa utaratibu huo,’’ alisema Naibu Waziri Mabula.


Waziri Mabula  alizitaka halmashauri zote zilizokopeshwa fedha na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja kuzirejesha kulingana na makubaliano ili kuwezesha halmashauri nyingine zenye uhitaji kukopa. Alisema halmashauri zitakazokaidi kuzirejesha fedha kwa wakati basi suala hilo litawasilishwa mamlaka husika ili wahusika wakatwe fedha hizo moja kwa moja.


Aidha Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa Hamid Njovu alimuahidi Naibu Wzairi wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa halmashauri yake itahakikisha inakamilisha kulipa deni hilo kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2020/2021.

Post a Comment

0 Comments