Spika aidhinisha Machi 8 kwa kura ya kutokuwa na imani na serikali


Spika wa bunge nchini Libya Aguila Saleh amesema kuwa bunge litazungumzia kuandaliwa kwa kura ya kutokuwa na imani na serikali mpya ya umoja wa taifa mnamo Machi 8.


Kupitia taarifa hapo jana jioni, Saleh amesema kuwa kikao cha bunge kitaandaliwa kuzungumzia kura hiyo mjini Sirte iwapo tume ya pamoja ya kijeshi itahakikisha usalama wa mkutano huo. 


Tume hiyo ya kijeshi inawaleta pamoja waakilishi watano kutoka kila upande. Saleh ameongeza kuwa iwapo hatua hiyo haitawezekana, kikao hicho kitaandaliwa katika makao ya bunge ya muda mjini Tobruk siku na wakati huo huo na kuongeza kuwa tume hiyo ya kijeshi itapaswa kuliarifu bunge mapema.


Waziri mkuu wa muda Abdul Hamid Dbeibah, siku ya Alhamisi alisema kuwa anakabiliwa na tarehe ya mwisho ya Ijumaa kuunda serikali yake kulingana na mpangilio wa Umoja wa Mataifa. 


Dbeibah amesema kuwa amewasilisha kwa Saleh "maono" ya mpangilio wa baraza la mawaziri ambalo litasaidia kuiongoza Libya kwenye uchaguzi wa Desemba na kwamba majina ya mawaziri waliopendekezwa yatafichuliwa bungeni wakati wa kura ya imani.

Post a Comment

0 Comments