TALIRI yajikita kutatua changamoto za wafugaji

 


Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima amesema utafiti wanaoufanya umejikita katika kutatua changamoto za mbegu bora za mifugo na mbegu bora za malisho kwa wafugaji ili sekta ya mifugo iweze kuchangia vyema katika pato la Taifa.

Dkt.  Kizima aliyasema hayo alipotembelea kukagua shughuli zinazofanywa na Kituo cha TALIRI Mpwapwa kilichopo Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma Februari 18, 2021.

Alisema kuwa lengo la utafiti wanaoufanya ni kuhakikisha wanapata mbegu bora za mifugo na kuzalisha mbego bora za malisho ya mifugo ambazo zitakazosaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa mbegu bora za mifugo zinazohimili mazingira yaliyopo na malisho inayoikabili nchi kwa sasa.

Aliongeza kuwa kwa sasa taasisi hiyo inaendelea na kufanya Tathmini ya ubora, ustahimilivu na makuzi ya malisho ya mifugo yatakayofaa kwa chakula cha kutosha kwa ajili ya mifugo.

Kwa mujibu wa Dkt. Kizima, matokeo yoyote ya utafiti lazima yabadilishwe kuwa biashara kwa sababu wafugaji wakifanya ufugaji unaoendana na mazingira yao itawasaidia kutengeneza uchumi na kuwaongezea tija katika ufugaji wao.

“Tafiti tunazozifanya zinalenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa mifugo ili mchango wa sekta ya mifugo uweze kuonekana katika uchumi wa kati,” alisema Dkt. Kizima

Dkt. Kizima alisema kuwa TALIRI imesambaza vituo vyake katika Kanda Saba nchini ili kuwa karibu na wafugaji kuwasaidia kutatua changamoto zao ili waweze kufanya ufugaji wenye tija.

Alisema vituo hivyo vipo katika Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Naye, Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa alisema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezihamasisha Halmashauri zote nchini kuanzisha mashamba darasa ya malisho ili wafugaji waweze kujifunza na kupata mbegu bora za malisho kwa ajili ya mifugo.

“Tunawahimiza wafugaji kuona umuhimu wa kulima malisho ili yaweze kuwasaidia kupata lishe ya uhakika kwa mifugo yao na pia kwa kulima malisho kutawapunguzia migogoro ya mara kwa mara kati yao na wakulima,” alisema Dkt. Mwilawa

Aliongeza kuwa wanawahamasisha wafugaji hususan walio katika nyanda kame wastawishe malisho ya mifugo wakati wa masika na kuyatunza ili yaweze kuwasaidia kulisha mifugo yao wakati wa kiangazi. 


Post a Comment

0 Comments