https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mahakama yatoa amri kuwalinda mashahidi kesi ya mauaji | Muungwana BLOG

Mahakama yatoa amri kuwalinda mashahidi kesi ya mauaji

 


Kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa ujangili raia wa Afrika Kusini, Wayne Derek Lotter imechukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu kutoa amri ya kulindwa, kutowekwa wazi kwa mashahidi wa kesi hiyo na taarifa zinazowahusu wao na familia zao.


Amri hiyo ya mahakama inalenga kuwalinda mashahidi hao katika kesi hiyo nyeti ambayo upande wa Jamhuri umedai wamekuwa wakitishwa.


Uamuzi huo umetolewa na Jaji mfawidhi, Lameck Mlacha kufuatia maombi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) yaliyosikilizwa upande mmoja, bila kuhusisha upande wa washtakiwa.


Katika maombi yake, DPP pamoja na mambo mengine, amedai mashahidi hao wamekuwa wakipata vitisho kutoka kwa washirika wengine wa mpango wa mauaji ya mwanaharakati huyo.


Jaji Malacha amekubaliana na DPP kuwa katika kesi hiyo kuna mazingira na taarifa za kutosha kumridhisha kukubali maombi DPP.


Amebainisha taarifa hizo kwa washtakiwa katika kesi hiyo ni sehemu tu ya ushirika wa uhalifu waliopanga na kutekeleza mauaji hayo na kwamba upelelezi umeibua mikakati ambayo imekuwa ikiendelea na kuainisha taarifa ambazo haziwezi kuwekwa wazi.


Akinukuu kesi moja iliyoamriwa nchini India miaka 150 iliyopita, Jaji Mlacha amesema, “mashahidi ni macho na masikio ya haki.”


Amesema bila mashahidi hakuna usikilizwaji kesi na hakuna haki na kwamba mashahidi lazima walindwe na si kudhurika au kuuawa na kwamba hata familia zao zinapaswa kutendewa hivyo.


“Mahakama na dola zinapaswa kuchukua jukumu thabiti kuhakikisha kwamba mashahidi na familia zao wanalindwa. Hii itahakikisha usikilizwaji sawa na kukuza utawala wa sheria,” amesema Jaji Mlacha.


Ametoa amri nane ikiwemo ile ya kutaka utambuzi wa mashahidi wa upande wa mashtaka usitolewe wakati wa ufungaji na uhamishaji wa kesi hiyo kutoka mahakama ya chini kwenda Mahakama Kuu kwa usikilizwaji.


Mahakama pia imezuia taarifa kuhusu maelezo ya mashahidi na nyaraka za mashahidi zisiwekwe wazi kwa sababu hiyo, washitakiwa watasomewa mashtaka na maelezo yaliyoandaliwa tu awali wa kesi dhidi yao Mahakama Kuu utafanyika katika chumba cha Jaji bila watu wengine kuruhusiwa


Amri hiyo imezuia uchapishaji au utolewaji wa taarifa zitakazowezesha utambuzi wa mashahidi, makazi na mahali walipo ndugu wa mashahidi wa upande wa mashtaka.


Pia mahakama hiyo imeamuru teknolojia ya video kupokea vielelezo na maelezo ya awali usikilizwaji kutokuwekwa wazi, mashahidi wa Jamhuri na familia zao kupewa ulinzi wakati wote wa usikilizwaji wa kesi hiyo hadi itakapohakikisha kuwa hakuna vitisho vyovyote.


Lotter alikuwa mkurugenzi na mwanzilishi mwenza wa shirika lisilo la kiserikali la PALMS Foundation lililokuwa linajishughulisha na mapambano ya ujangili.


Aliuawa Agosti 16, 2017 kwa kupigwa risasi na watu waliomvamia akiwa kwenye teksi na mwenzake katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selaissie, Masaki, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.


Watu 22 wameshitakiwa kwa mauaji hayo wakiwemo raia wawili wa Burundi. Washitakiwa hao ni Khalid Mwinyi ambaye ni Meneja wa Benki ya Backlays, mkazi wa Mikocheni B; Rahma Almas, mkazi wa Mbagala B na  Nduimana Ogiste, maarufu kama mchungaji na raia wa Burundi.


Wengine ni Godfrey Salamba mkazi wa Kinondoni Msisiri A; Innocent Kimaro,  mkazi wa Temeke Mikoroshini; Chambie Juma Ally,  mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa benki ya NBC; Robert Mwipyana, mkazi wa Temeke Mikoroshini na Allan Elikana Mafue;


Pia yumo Ismail Issah  Mohammed (Machipsi); Leornad Phillipo Makoi; Amini Abdallah Sham; Ayoub Selemani Kiholi; Joseph Alexander Lukoa;  Gaudence James Matemu ; Abuu Omary Mkingie na  Habonimanda Augustine Nyandwi (pia raia wa Burundi);


Vilevile kuna Abdallah Salum Bawaziri, mkazi wa barabara ya sita jijini Dodoma; Michael Dauv Kwavava; Emmanuel Thomas Sonde; Kelvin Athanas Soko; Samia Saleh  Hujat na Almasi Swed maarufu Malcolm.


Akiwasomea maelezo ya kesi Jumatatu Machi mosi, 2021 wakati wa uhamishaji kesi hiyo, Wakili wa  Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amedai washtakiwa hao walikula njama za mauaji hayo kwa nyakati kati ya Julai mosi na Agosti 16, 2017 katika vikao walivyokaa jijini Dar es Salaam na Ausha.


Amedai katika vikao hivyo walikubaliana kununa silaha za kutekeleza mauaji hayo nje ya nchi ambapo mshtakiwa wa tatu ambaye ni raia wa Burundi alitumia Sh3 milioni kununua bunduki na kisha kuzisafirisha kuzileta nchini kwa njia haramu.


Siku ya tukio, Lotter na wenzake walisafiri kutoka Arusha kuja Dar es Salaam na kwamba mmoja wa washtakiwa aliyekuwa Arusha aliwajulisha wenzake waliokuwa Dar es Salaam na mshtakiwa wa 18 ambaye ni dereva teksi alipewa jukumu la kuratibu kuwasili kwao Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).


Wakili Wankyo alidai kuwa mshtakiwa 18 kwa kuwa alikuwa mwenyeji wa mwanaharakati huyo katika mizunguko yake alimchukua kwenye gari lake kutoka awanjani hapo na kumpeleka Masaki ambapo aliwasiliana na wenzake wakapanga kutekeleza mauaji.


Washitakiwa wanadaiwa kuwapora kompyuta mpakato (laptop) tatu na simu kisha mshtakiwa tatu alimpiga Lotter risasi kutumia bunduki aina ya UZI na kumuua.

Post a Comment

0 Comments