Kombora la kutungua ndege la Syria laanguka karibu na kinu cha nyuklia cha Israel


Kombora moja la kuangusha ndege la Syria limelipuka kusini mwa Israel , takriban kilomita 30 kutoka kinu kimoja cha siri cha kutengeneza nyuklia .

Ving'ora vilisikika kabla ya mlipuko huo mkubwa kusikika katika eneo la Dimona. Hakuna majeraha au uharibifu ulioripotiwa.

Jeshi la Israel limesema kwamba kombora hilo ni mojawapo ya makombora kadhaa ambayo yalirushwa kulenga silaha moja ya kutungua ndege.

Silah hiyo ilijibu kwa kushambulia silaha za kulinda anga ya taifa hilo.

Jeshi la Syria lilisema kwamba makombora ya Israel yalilenga maeneo karibu na mji mkuu wa Damascus.

Iran kulipiza kisasi shambulio dhidi ya mtambo wake wa nyuklia

''Baadhi ya makombora yalitunguliwa na kuangushwa , lakini wanajeshi wanne wa Syria walijeruhiwa na kuna baadhi ya maeneo yalioharibiwa'', liliongezea

Shirika la haki za kibinadamu nchini Syria The Syrian Observatory for Human Rights, lenye makao yake Uingereza liliripoti kwamba makombora ya Israel yalishambulia kambi za kulinda anga ya taifa hilo katika mji wa Dumayr, takriban kilomita 40 kaskazini mashariki mwa Damascus.

Eneo hilo linaaminika kuwa lenye makombora ya Iran yanayomilikiwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran pamoja na jeshi la Syria katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Hivi majuzi , iliripotiwa kwamba usalama wa maeneo ya Dimona na bandari ya Eilat nchini Israel ulikuwa umeimarishwa iwapo kungetokea mashambulizi yanayotekelezwa na vikosi vinavyoungwa mkono na Iran katika eneo hilo ikiwemo vile vilivyomo nchini Syria.

Hali ya wasiwasi inaendelea kutanda kati ya maadui hao wawili huku Iran ikilaumu Israel kwa kutekeleza kitendo cha hujuma dhidi ya kinu chake cha kuzalisha madini ya Uranium cha Natanz mapema mwezi huu.

Israel haikusema kwamba ilihusika na shambulio hilo.

Kinu cha nyuklia cha Israel kilichopo Dimona kinadaiwa kutengeneza silaha.

Israel haijathibitisha au kukana kwamba inamiliki silaha za kinyuklia chini ya sera yake yenye utata.

Post a Comment

0 Comments