Dhana ya Uchumi wa Buluu inavyokwenda kuwafaidisha Wazanzibar

 


Na Thabit Madai, Zanzibar.

SI Ajabu tena kusikia neno Uchumi wa Buluu visiwani hapa ambapo ikiwa na maana kuwa ni shughuli zote za Uendelezaji na ukuzaji wa uchumi  kwa kupitia matumizi bora ya Rasilimali zote muhimu za bahari.

Dhana nzima ya Uchumi wa Buluu ni pana ambayo imebeba shughuli zote za msingi zinazofanywa katika bahari kama vile, uvuvi wa aina mbalimbali ukiwemo wa kibiashara na usio wa kibiashara katika kina kirefu na kifupi cha maji, Shughuli za usafirishaji  Baharini, Shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini na mafuta Baharini.

Hali kadhalika shughuli zote za starehe na michezo kando kando mwa bahari, Shughuli za bandari na upana wake pamoja na Masuala mengine kama vile ujenzi wa vyombo vya baharini Meli, Boti na shughuli za elimu na tafiti kuhusu bahari.

Hakuna asiejua tena kuwa uchumi wa Buluu unafaida kubwa sana katika ukuzaji wa Uchumi wa nchi yoyote ile  ambapo huongeza pato la taifa na pato la mwananchi mmoja mmoja endapo sekta hii itaangaliwa kwa jicho la kipekee kabisa.

Katika Makala hii itazungumzia juu ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia Mamlaka zake pamoja na maoni mbalimbali ya wadau juu ya ukuzaji wa sekta hii.

MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BAHARI KUU (DSFA)

Akizungumza na Makala haya, Kaimu Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu, Emmanuel Sweke alisema kuwa Mamlaka imejidhatiti kwa kiasi kikubwa kuendeleza kwa vitendo Sera ya Serikali ya awamu ya nane ya kukuza Uchumi kupitia Bahari.

Sweke alisema tayari mamlaka kupitia Serikali kuu imefanya mapitio na kurekebisha baadhii ya Sheria, Kanuni na taratibu mbalimbali zinazotoa fursa kwa wadau mbalimbali kujitokeza katika kuwekeza kupitia bahari kuu ambayo ndio msingi mkuu wa uchumi wa Buluu.

“Sisi kama Mamlaka tayari tumeweka sheria, Kanuni na taratibu nzuri ambazo zinawawezesha wadau kuja kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu ukizingatia kuwa moja ya nyenzo ya uchumi wa buluu ni uvuvi wa bahari kuu,”alilieleza

Alisema kwamba, ili kukuza uchumi wa Buluu inatakiwa kuwekwe mazingira rafiki kwa wavuvi wadogo wadogo wa ndani pamoja na wawekezaji wa ndani  katika sekta nzima ya uvuvi.

“Katika kuwavutia wawekezaji wa ndani na hata wawekezaji wa Nje, tumeweka motisha mbalimbali kama vile kuwapunguzia bei za leseni kwa wawekezaji wazawa pamoja na muda wa Leseni ambapo wawekezaji wazawa wataweza kukata Leseni kuanzia miezi 3 na kuendelea, huku Mwekezaji mgeni anatakiwa kukata kuanzia miezi 6 na miezi 12,”alifafanua Sweke.

Alisema pia Wazawa wamewekewa fursa ambayo wanaweza kuingia ubia na watu wengine wenye uwezo katika kuwekeza katika uvuvi wa bahari Kuu na kuvua samaki na kunufaisha taifa kwa ujumla.

“Hii yote inatokana na kuwa tumekusudia kuendana na sera ya Serikali ya kukuza uchumi wa Buluu unapowainua wavuvi wadogo wadogo na kuweka mazingira kwa wawekezaji kuja kuvua katika bahari kuu unakuza uchumi na kipato kupitia bahari ambayo imetuzunguka,” alieleza.

Aidha alieleza kuwa tayari Mamlaka imeshafanya utafiti maalumu wa kutambua maeneo mbalimbali ya ukanda wa bahari yenye samaki wa kutosha kwa lengo la kuwaondolea usumbufu na gharama kwa wavuvi.

“Kupitia wadau tumefanya utafiti wa kujua maeneo hasa yenye samaki wa kutosha ambapo tunawaelekeza wavuvi sehemu za kwenda kuvua, hii inasaidia kuwaondolea usumbufu pamoja gharama kubwa ambayo wangeweza kuitumia katika kutafuta samaki,”alieleza.

WIZARA YA UCHUMI WA BULUU

Abdallah Hussein Kombo ni Waziri wa Wizara hiyo ambao alieleza  kuwa Wizara miandaa mikakati mahsusi ya kukabiliana na changamoto yoyote ile itakayojitokeza wakati Serikali ikitekelza Sera yake ya kukuza Uchumi kupitia Uchumi wa Buluuu.

Aliongeza kwamba Wizara imeanza na mkakati wa kukabiliana na changamoto ya uchache wa wataalamu wa kuzihudumia sekta zilizomo katika wizara hiyo ya uchumi wa Buluu.

“Tatizo hilo linazikabili nchi nyingi zinazopatikana na bahari, hivyo kuna haja ya kuwekwa mikakati itakayoimarisha uchumi kupitia sekta mbali mbali ikiwemo ya uvuvi ambao ndio shughuli mama katika uchumi wa Buluu,” anaeleza.

Waziri alibaisha kwamba, ili kufikia azma ya Zanzibar kunufaika na uchumi wa buluu, lazima sekta hiyo isimamiwe vyema na kuwekwa mkazo katika vipaumbele vya serikali ya awamu ya nane.

"Dhana ya uchumi wa bluu ni mtambuka na inahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu, ninawaomba tuendelee kuimarisha mashirikiano baina ya serikali na sekta binafsi sambamba na wadau wengine wa maendelo," anaeleza Kombo.

Waziri Kombo alieleza kwamba iwapo  changamoto zote   zitafanyiwa kazi kimkakati, uchumi wa buluu utakuwa na tija kwa Zanzibar na watu wake na kuelekeza mbinu za utekelezaji ikiwemo ya kuzifanyia mapitio sera na sheria zilizopitwa na wakati sambamba na kuwekwa mpango mzuri wa matumizi ya bahari (Special planning).

“Hatuwezi kuwa na uchumi wa buluu tukaitumia bahari kama shamba la bibi, lazima tuwe na mpango madhubuti utaonyesha namna gani tutakuwa na nia ya kuitumia bahari yetu,” anasisitiza.

TUME YA MIPANGO

Saleh Saad Mohammed afisa kutoka Tume ya Mipango Serikali alisema kuwa, iwapo Serikali itajidhatiti katika kutekeleza kwa vitendo dhana nzima ya Uchumi wa Buluu, kuna fursa nyingi zitaibuliwa na kuimarisha uchumi wa Zanzibar na watu wake.

"Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na ujenzi wa bandari ya uvuvi baina ya serikali na sekta binafsi, ujenzi wa sehemu ya kuhifadhia samaki na kujenga kiwanda cha uzalishaji barafu itakayotumika kuhifadhia samaki na mazao mengine ya baharini," anaeleza Mohammed.

Aidha alieleza kwamba wakati umefika sasa Wazanzibar na waatanzania kwa ujumla kuanza  kuvua katika bahari kuu ili kujiongezea tija na faida.

"Zanzibar ina rasilimali kubwa ya wavuvi wadogo wadogo wenye ujuzi lakini wanakosa mbinu na uwezo wa kufika katika maji makubwa hivyo watakapowezeshwa pamoja na kujengewa uwezo, watavua katika bahari kuu na kuongeza kipato chao," anabinisha.

WAVUVI

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wavuvi Kojani,Omar Mohamed Ali anasema kwamba kwa sasa Wazanzibar wategemee bahari kama sehemu kimbilio salama, ambapo waipongeza Serikali ya awamu ya nane kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha uchumi wa Nchi unatokana na bahari.

“Nampongeza Dk Hussein Ali Mwinyi Rais wetu kwa kuonesha juhudi za kuboresha sekta ya uvuvi kutokana na ukweli kwamba jiografia ya Zanzibar imezungukwa na bahari na wananchi wake wanategemea sana sekta nzima ya Uvuvi.

Aidha Khamis Mussa Makame Mvuvi kutoka Bububu anaeleza kuwa serikali imejidhatiti kuongeza thamani ya shughuli za uvuvi na matumizi ya bahari hivyo anaona kuwa ajira nyingi kwa vijana zitazalishwa.

“hapo nyuma ukiwa mvuvi  ni kazi ya kudharaulika ila sasa uvuvi unaonekana ni nyenzo nzima ya kukuza na kuboresha uchumi wan chi na kipato cha nchi,” anaeleza.

Hata hivyo anaeleza kuwa ni wakai wa Serikali kushirikiana na wananchi bega kwa bega katika kuhakikisha sera yake ya uchumi wa Buluu inakuwa ipasavyo na kuwanufaisha wananchi wake.

WANASIASA WANAMTAZO GANI JUU YA UCHUMI WA BULUU.

Ameir Hassan Ameir Katibu wa Chama cha Demokrasia Makini alisema kuwa Serikali kupitia wadau wake mbalimbali inapaswa kujipambanua kwa kina juu ya sera ya Uchumi wa Buluu ambapo anaamini kuwa Kuna nafasi kubwa na nzuri ya kuifanya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuwa na uchumi uliobora kupitia bahari.

“ Kwa mfano hapa kwetu Zanzibar, Sekta nzima ya uvuvi  huchangia asilimia 2.6 ya pato ghafi la Zanzibar ambapo hutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya laki mbili ndani a visiwa hivi huku zaidi ya watu laki  Nne wakiwa wanategemea sekta hii,” anasema Ameir.

 Aliongeza kuwa,Kuimarika kwa sekta nzima ya uvuvi na bahari  hupelekea kukuwa kwa uchumi wa nchi pamoja wananchi kwa ujumla hivyo anashauri serikali kuendelea kuweka mipango iliyothabiti katika kutekeleza sera yake ya kukuza uchumi kupitia Bahari (Blue Economy).

Nae Katibu Mkuu wa Chama cha UPDP Hamad Ibrahimu alieleza kuwa ili kukuwa mapema kupitia uchumi wa Buluu Serikali inapaswa kudhibiti uvuvi haramu pamoja na kuwainua wanawake kwa kuwapatia nyenzo mbalimbali zitakazo  wawezesha kumudu shughuli zao za baharini.

“Asilimia 2 ya wanawake duniani kote hujishughulisha na shughuli mbalimbali za bahari  hivyo serikali ikiweka mazingira mazuri kwa wanawake hawa katika kujiendeleza na shughuli zao huchangia kukua na kukuza sekta ya bahari pamoja na kudhibiti uvuvi haramu,” anaeleza.

Alieleza  kwamba ili kuwa na uchumi endelevu na kuenda sambamba na mataifa mengine Serikali inapaswa kuwa na mipango imara inayotekeleza katika uchumi wa Buluu ambao ndio kiini cha uchumi wa Kileo.

RAIS DK. HUSSEIN ALI MWINYI

Rais Dk.Hussein ali mwinyi mapema majipambanua yeye na Serikali yake kwamba dhamira yao ni kujenga  Zanzibar mpya kwa kupitia uchumi wa kisasa, Uchumi wa Buluuu  (Blue Economy).

Katika moja ya hotuba zake, Dk Mwinyi  Alisema kuwa Uchumi wa Buluu ama uchumi wa bahari unafungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbali mbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

Aliongeza kuwa uchumi wa Buluu haukamiliki bila ya kuwepo kwa Bandari za kisasa zenye ufanisi wa hali ya juu hivyo lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga bandari kubwa za kisasa ambazo zitatoa huduma kwa wavuvi na kuchangia kukuza uchumi wa Zanzibar Mpya.

NINI KIFANYIKE KATIKA KUKUZA SEKTA HII

Ni vizuri sana kwa Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar  kuiona dhana ya uchumi wa buluu kama fursa kwa ajili ya fikra na mabadiliko ya kiuchumi, Zipo nchi mbalimbali zilizojikita katika uchumi wa buluu kama jukwaa la kujikomboa na kujiendeleza kiuchumi.

Kati ya nchi hizi ni zile za umoja wa nchi ishirini zinazooshwa na Bahari ya Hindi ikiwemo Tanzania. Umoja huu unaitwa Indian Ocean Rim Association (IORA). Mwandishi wa makala haya ni mdau wa umoja huu kupitia jukwaa la wanataaluma.

Uchumi wa buluu ni kati ya maeneo yanayoangaliwa kwa jicho la kipekee katika umoja huu. Kwa Afrika, ni Afrika Kusini tu iliyo mbele zaidi katika kuendeleza na kutumia dhana ya uchumi wa buluu kama mkakati wake wa maendeleo ya uchumi.

Ni vizuri kwa Zanzibar kujifunza namna ambavyo nchi nyingine zinavyotumia dhana hii kama fursa ya uchumi si kwa mtu mmoja mmoja tu bali kwa Taifa kwa ujumla.


 

Post a Comment

0 Comments