Kamati ya Maendeleo Jimbo la Mpendae yakabidhi Msaada wa Gari la kubebea Wagonjwa


Na Thabit Madai, Zanzibar.

MBUNGE wa Jimbo Mpendae Taufiq Turky kwa kushirikiana na kamati ya maendelo ya jimbo hilo wamekabidhi gari moja ya kubebea wagonjwa (AMBULANCE) pamoja na vifaa tiba katika hospitali ya Mpandae Mjini Unguja ikiwani utekelezaji wa ahadi kwa wananchi.

Msaada huo wenye thamani ya shilingi Milioni 45 ulikabidhiwa kwa Waziri wa Afya,Ustawi Jamii, Wazee, Jinsia na watoto Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui ambapo hafla ya makabidhiano ilifanyika huko Mpendae Unguja.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mbunge wa Jimbo hilo Taufiq Turky alisema kuwa Msaada huo ni utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi CCM, kwa kuwapatia wananchi huduma zilizobora za afya na karibu na makaazi yao.

“Nina furaha kubwa sana siku ya leo kwa kukabidhi gari hii pamoja na vifaa tiba ambapo itawasaidia wananchi wetu wa Mpendae pamoja na wale wote majimbo jirani ukizingatia Hospitali hii inahudumia watu kutoka maeneo tofauti ya Zanzibar,” alieleza Turky.

Alieleza kuwa, katika Jimbo la Mpendae kuna kesi nyingi zinaripotiw a za wagonjwa kutofika kwa wakati hospitali kutokana na uhaba wa gari ya kubebea wagonjwa na kusababisha maradhara ikiwemo vifo.

“Tumeamua kuanza na Gari ya kubebea wagonjwa kutokana na ripoti nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wagonjwa kushindwa kufikishwa hospitali kwa wakati na kupata madhara makubwa,”alieleza 

Katika hatua nyingine Turky aliwaomba wananchi jimboni hapo kuunga mkono jitihada za kamati maendeleo ambayo inaongozwa na Mbunge, Muakilishi pamoja na madiwani katika kuleta maendeleo sambamba na kutekeleza ahadi na Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM.

Nae Mwakilishi wa Jimbo hilo, Shabani Ali Othman alisema kuwa msaada huo walioutoa jimboni hapo unakwenda kupunguza ahadi zao walizotoa wakati wa kampeni na kuwasaidia moja kwa moja wananchi wa Mpendae.

“Leo ni siku kubwa sana, nina furaha kuona Kwa kipindi kisichozidi miezi 6 tunatekelza Ilani pamoja na kutekeleza ahadi zetu kwa wananchi tuliowahidi ambapo unakwenda kuwasaidia,”alisema Mwakilishi huyo.

Mapema akipokea msaada huo Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii,Wazee,Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuwasaidia wananchi kupata huduma zilizokuwa bora.

Alisema, Serikali itaweka mazingira yaliyorafiki ili wadau mbalimbali wajitokeze katika kutoa misaada mbalimbali yenye lengo la kuwasaidia wananchi.

“Sisi kama serikali tutaendelea kuunga mkono jitihada kama hizi kwa wadau katika kuwasaidia wananchi kupata huduma zilizobora na maendeleo katika jamii,”alieleza

Pia aliwataka kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Mpendae kuongeza kasi ya kutekeleza ahadi walizozitoa kwa wananchi bila ya kujali siasa,jinsia na maeneo wanayotoka.

“Ni jambo zuri na la mfano mumelifanya munatakiwa kushirikiana na wananchi wote katika kuwaletea maendeleo bila ya kujali vyama vya Siasa, Jinsia na maeneo wanayotoka,”aliwaeleza.

Katika hatua nyingine Mbunge wa Jimbo hilo kwa kushirikiana na kamati za Maendeleo wamezindua rasmi zoezi la ugawaji wa futari kwa wananchi wote jimboni hapo ambapo ikiwa ni muendelezo wa Kumuenzi aliekuwa mbunge wa Jimbo hilo Salim Turky.

 

Post a Comment

0 Comments