Miradi minne ya umeme kumaliza Vijiji na mitaa yote mkoa wa Dodoma


Na Ezekiel Mtonyole - Kongwa.

Serikali imesema inatekeleza miradi ipatayo minne ya umeme katika Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuhakikisha maeneo yote yanapata umeme na kuwawezesha wananchi kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zitakazo wezesha kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamebainishwa Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma na  Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Medard Kalemani wakati akiwasha umeme katika kijiji cha Makutupa Wilayani Kongwa akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo na watumishi wa TANESCO.

Amesema endapo miradi hiyo ikikamilika itawezesha Vijiji mbalimbali kupata nishati ya umeme hali itakayosisimua shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.

Waziri Dkt Kalemani ametaja miradi inayotekelezwa kuwa ni mradi wa kusambaza umeme vijijini  unaoendelea sasa wa awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo, mradi wa kupeleka umeme vitongojini, mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo yaliyo karibu na mitaa mijini (Peri-urban) na miradi inayotekelezwa na TANESCO.

“Kwa Mradi wa kusambaza umeme vijijini Dodoma, Serikali imetoa takriban shilingi bilioni 60, mradi wa kupeleka umeme vitongojini Serikali imetoa shilingi bilioni 48.3, kwa mradi wa Peri-Urban Serikali imetoa shilingi bilioni 23 na mradi mwingine unatekelezwa na fedha kutoka TANESCO kama ilivyo hapa Makutupa.” amesema Dkt.Kalemani

Dkt Kalemani amebainisha kuwa katika kazi ya usambazaji umeme katika vijiji mbalimbali Mkoa wa Dodoma takribani vijiji  467 vimeshasambaziwa umeme, kati ya vijiji 581 vilivyopo ambayo ni zaidi ya asilimia 81 huku akibainisha vijiji vilivyobaki miradi inaendelea.


Waziri Dkt Kalemani amebainisha kuwa kwa Wilaya ya Kongwa ni vijiji vinne (4) tu ndivyo havijafikiwa na nishati ya umeme Kati ya vijiji 87 vilivyopo katika Wilaya ya Kongwa ambapo ndani ya miezi mitatu vitafikishiwa umeme.

Akiwa wilayani Kongwa, Waziri wa Nishati pia ametembelea eneo la Mbande ambalo wananchi wake wamekuwa wakilalamika kuwa kuna nguzo za umeme zilizosimikwa muda mrefu bila wananchi hao kuunganishiwa umeme.

Akiwa katika eneo hilo, Dkt.Kalemani amewahidi kuwa, Mkandarasi, kampuni ya Derm Electric ataanza kuwaunganishia umeme wananchi kuanzia Ijumaa ya tarehe 7 Mei, 2021.

Akizungumza na wananchi wa Makutupa na Mbande, Dkt.Kalemani amewasisitiza kutumia umeme kwa matumizi mbalimbali kwani Serikali inatumia fedha nyingi kufikisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kupunguza gharama za uunganishaji ili kila mtanzania atumie nishati hiyo muhimu.

Katika hatua nyingine Dkt.Kalemani amesema kwa vijiji 1974 ambavyo bado havijasambaziwa umeme kwa nchi nzima kati ya vijiji 12,268, wakandarasi wa kusambaza umeme kwenye vijiji hivyo wameshapatikana na wataingia katika maeneo ya kazi wiki ijayo.

 

Post a Comment

0 Comments