Rais Samia Suluhu Hassan amkabidhi nyumba ya kuishi Mhe. Rais Mstaafu Kikwete

Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amemkabidhi nyumba ya kuishi Rais mstaafu, Jakaya  Kikwete iliyojengwa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Nyumba hiyo imejengwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ikiwa ni utekelezaji wa kifungu namba 12 cha sheria ya mafao ya hitimisho la kazi kwa viongozi wa siasa sura ya 225 na marejeo ya mwaka 2020.

Kifungu hicho kinaelekeza kuwa  pamoja na stahili nyingine za matunzo ya viongozi wakuu wastaafu, rais mstaafu anastahili kujengewa nyumba ya kuishi yenye hadhi ya rais.

Akizungumza baada ya kukabidhi nyumba hiyo leo Jumapili Mei 9, 2021,   Rais Samia amemhakikishia  Kikwete kuwa Serikali itaendelea kumtunza yeye na viongozi wengine wastaafu kama inavyoelekezwa katika sheria.

Amebainisha kuwa Serikali itafanyia kazi uboreshaji wa sheria hiyo pamoja na kuhakikisha wajane,  wagane wa viongozi wanatunzwa.

Rais Samia ametumia fursa hiyo kumuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mohamed Mchengerwa kuanza maandalizi ya kutimiza haki zote anazostahili aliyekuwa rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli.

Naye Mchengerwa amesema nyumba hiyo ni ya tatu kukabidhiwa ikitanguliwa na nyumba ya Rais mstaafu Hayati Benjamin  Mkapa na Rais mstaafu,  Ali Hassan Mwinyi.

Amesema nyumba ya  Baba wa Taifa,  Hayati Julius Nyerere ilijengwa na kukabidhiwa  na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika shukrani zake, Kikwete  aliyeongozana na mkewe, Salma ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutekeleza takwa hilo la kisheria, ameishukuru TBA kwa kukamilisha ujenzi tangu ulipoanza mwaka 2018.

Kikwete pia  amempongeza Samia kwa uongozi wake tangu alipopokea kijiti kufuatia kifo cha  Magufuli akieleza kuwa  nchi imetulia mambo yanakwenda na watu wana matumaini naye.

 

Post a Comment

0 Comments