SMZ ina azma ya kuimarisha viwango vya mishahara

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ina azma ya kutekeleza utaratibu wa kuimarisha viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wa ‘Kada ya kati’, pale hali ya uchumi utakapozidi kuimarika.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil Kikwajuni Jijijini Zanzibar. 

Amesema wafanyakazi wa eneo hilo ni muhimu katika maendeleo ya Taifa kwa vile ndilo lenye wataalamu, ikiwemo walimu, wafanyakazi wa afya na wengineo ambapo hivi sasa wamekuwa wakilipwa mishahara duni. 

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba ilikuwa na nia njema ya kuimarisha  mishahara kwa wafanyakazi wa ngazi zote kwa awamu tatu, hata hivyo hatua hiyo ilishindwa kukamilika kutokana na kuibuka kwa ugonjwa Corona na kuathiri ukusanyaji wa mapato na hivyo hivyo utaratibu huo kuishia kwa kuimarisha viwango vya mishahara ya kima cha chini hadi kufikia shilingi 300,000/- 

Aidha, alisema Serikali inalenga kuangalia upya utaratibu wa malipo ya kiunua mgongo kwa wafanya kazi waliostaafu (maarufu kwa jina la vikokotoo) ikiwa na lengo la kuwanufaisha wafanyakazi, wakati huu ambapo wafanyakazi na wastaafu wengi wanalalamikia utaratibu huo.

 

Post a Comment

0 Comments