May 9, 2021

Tumieni masoko ya Madini nchini kuuza Madini - Waziri Biteko

  Muungwana Blog 2       May 9, 2021

 


Wachimbaji wa Madini wametakiwa kutumia masoko ya madini yaliyoanzishwa kote nchini katika kuuza madini wanayozalisha katika migodi yao.

Mwito huo umetolewa na Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko jana tarehe 8 Mei 2021 wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa Madini Mkoa wa Geita.

Waziri Biteko amewataka wachimbaji hao kujiepusha na utoroshaji wa madini, sambamba na kutoa taarifa pale wanapoona kuna mchimbaji anakwenda kinyume na taratibu zilizowekwa na wizara ya madini na serikali kwa ujumla.


Amewataka kuzingatia usalama mahala pa kazi pamoja na utunzaji wa mazingira ili fedha wanayoipata kutoka kwenye madini wanayozalisha kuitumia wakiwa na afya njema.

"Fuateni Sheria, Kanuni,  Taratibu na Miongozo inayosimamia Sekta ya Madini ili kujiepusha na changamoto zinazoweza kujitokeza ikiwemo kuwekwa kizuizini pindi wanapobainika kujihusisha na utoroshaji wa wizi wa madini" Alikaririwa Mhe Biteko

Waziri Biteko amesema kuwa lengo la msingi la kutoa mafunzo hayo ni kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini nchini kuwawezesha kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha ili waweze kufanya uchimbaji endelevu na wenye tija. 

"Hii itachangia katika kuongeza uzalishaji kutoka kwa wachimbaji wadogo na hivyo kuongeza mchango wao katika pato la Taifa ambao kwa hivi sasa bado ni mdogo. 

Ndugu washiriki wa mafunzo, Nitoe rai kwenu kutumia vyema fursa hii mliyoipata ya kukutana na wataalamu wa GST ili mjadili kwa kina mambo yote yanayohusiana na mada kuu pamoja na mambo mengine yanayolenga kuboresha kazi zenu za utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini wenye tija" Amesisitiza Waziri Biteko

Amesema kuwa ni matarajio yake kuwa mafunzo hayo pamoja na kitabu cha mwongozo yatawajengea uwezo ili kuendeleza ukuaji wa Sekta ya Madini na kuongeza pato la Taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Robert Gabriel ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa usimamizi mzuri wa sekta ya madini na hivyo kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi Kituo cha Uwekezaji (EPZA) mkoani Geita.

"Geita imebadilika kutokana na madini, hata hapa tulipo ni matokeo ya rasmilimali ya madini tuliyonayo ambapo mpango wetu pia ni kulifanya eneo hili kuwa na huduma zote ili mwananchi akija apate mahitaji yote muhimu" Ameeleza Mhe Gabriel.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Bi Yokbeth Muyumbilwa amesema kuwa Taasisi hiyo imepitia mabadiliko mengi ya kimuundo ambapo miongoni mwa majukumu yake ya msingi ni kusaidia wachimbaji wadogo kwa kufanya utafiti na kutoa mafunzo ya kuboresha uchimbaji na uchenjuaji wa Madini.


logoblog

Thanks for reading Tumieni masoko ya Madini nchini kuuza Madini - Waziri Biteko

Previous
« Prev Post

No comments:

Post a Comment