Balozi wa Umoja wa Ulaya aridhishwa na ushiriki wa wananchi katika mradi wa Viungo Zanzibar

Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania Manfredo Fanti ameleza kufurahishwa kwake na utekelezaji wa mradi wa Viungio visiwani Zanzibar na kusema kuwa ana matumaini makuwa mradi wa Kilimo cha mboga mboga, matunda na viungo utapunguza na hata kundoa  umasikini kwa wakulima wengi visiwani hapa.

Aliyasema hayo wakati wa ziara maalumu ya kutembelea baadhi ya mashamba ya wakulima katika shehia ya kizimbani na Biguni Unguja.

Alisema kilimo hicho ni miongoni mwa sekta muhimu ambayo ikitumiwa vyema itaweza kubadilisha maisha ya wakulima kwani wataweza kuzalisha kwa wingi, mazao yenye ubora na kupata soko la uhakika, hivyo amewataka wakulima hao kutokata tamaa na waendelee kuitumia fursa zinazopatikana kupitia mradi wa viungo.

Sambamba na hilo Balozi huyo amesema ushiriki mkubwa na utayari wa kujifunza waliouonesha wakulima wengi  unatia moyo na hivyo anaamini kwamba elimu waliopata wataitumia vyema kuendeleza kilimo chao kwa manufaa yao jamii, na taifa kwa ujumla. 

Aidha aliwataka wanufaika wa mradi  kuitumia fursa hiyo kama sehemu muhimu ya kujifunza na kuongeza uelewa kupitia aina mbali mbali mpya za kilimo ambazo hazikuwa zikitumiwa awali.

Baadhi ya wanufaika wa mradu huo Haji Abdallah Abeid ambae ni mkulima wa Vanila amesema elimu aliyoipata kupitia mradi wa viungo imemsaidia kuimarisha kilimo chake kwani ameanza kuona mabadiliko makubwa jinsi ya ulimaji wake kuanzia utayarishaji wa shamba, upandaji na anaamini atavuna mazao mengi na bora.

‘’Nimefanya shughuli za kilimo hiki kwa miaka mingi lakini kwa njia za kienyeji ambazo hazikuniwezesha kupata mafanikio ninayoyatarajia, lakini sasa kupitia elimu hii na utaalamu tunaoupata kutoka mradi wa viungo ninaamini ndoto yangu itatimia’’ alisema Haji bwana Adballah Abeid.

Alieleza kuwa kupitia mradi huo wa viungo amejifunza njia mpya za kilimo hicho cha vanilla na tayari ameanza kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuanzisha shamba jengine jipya ambalo tayari ameotesha miche zaidi ya 200.

Amefafanua kuwa kupitia mashamba darasa yanayoanzishwa kila shehia na mradi wa viungo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kujifunza mbinu mbalimbali ambazo zitaleta mafanikio makubwa  kwa wakulima  wa mboga mboga, matunda na viungo ambao ndio wanufaika wa mradi huo.

Akizungumzia kuhusu hali ya soko la vanila alisema kwa sasa kilo moja ya vanila wanauza kwa bei ya shilingi milioni moja na laki sita hivyo kupitia mradi huo anaimani soko la bidhaa hio litakua zaidi kwani wataongeza uzalishaji na ubora wa vanila.

Kwa upande wake mkulima wa matunda shehia ya Binguni Namri Najim alisema mfupo mpya wa  kilimo unaozingatia elimu utaleta tija kwao na kuzalisha bidhaa nyingi zaidi.

Mkulima huyo ambae anaejihusisha na kilimo cha pesheni na mapapai anasema pia kupitia mfumo huo watakua na uhakika wa masoko kutokana kuzalisha bidhaa bora zenye kiwango zinazohitajika ndani ndani na  nje ya Zanzibar.

Sambamba na hayo alisema miongoni mwa faida nyengine ya mradi huo umewasaidia kujikusanya kama kikundi na kufanya kazi kwa pamoja ambapo kabla ya elimu hio hawakua na taaluma za kuanzisha vikundi na kila mmoja alikua anafanya shughuli za kilimo kivyake.

Kwa upande wake Meneja mkuu wa utekelezaji mradi huo Amina Ussi Khamis amesema ujio wa Balozi kutembelea mradi huo una manufaa makubwa kufuatilia kile ambacho wamewekeza kwa nia ya kuwasaidia wananchi wa Zanzibar na Serikali yao.

Alisema anaamini wakulima wangi wataitumia fursa hiyo na kuwataka  waongeze kasi ya kujifunza zaidi kupitia mashamba darasa yaliopo katika shehia zao kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora sambamba na kuanzisha mayamba yao wenyewe kwa kila mnufaika.

Pamoja na hayo Meneja huyo alisema mradi huo wa Viungo upo wazi na wapo taayari kumsaida kila mkulima awe mmoja mmoja ama vikundi walio tayari na wenye muelekeo wa kutaka kuzalisha bidhaa nyingi zaidi.

Mradi huo wa VIUNGO unaofadhaliliwa wa umoja wa Nchi za Ulaya (EU) unatekelezwa kwa miaka mine visiwani Zanzibar katika shehia 60 za Unguja na Pemba ambao umelenga kuwafikia wanufaika  wapatao 57,974 na unatekelezwa kwa mashirikiano ya ya taasisi ya PDF,CFP na TAMWA-ZNZ.

 

Post a Comment

0 Comments