Kufuatia ujenzi holela wa vibanda vya Biashara katikati ya Jiji

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeanza kuwaelimisha wafanyabiashara ndogondogo kutojenga vibanda vya kudumu katikati ya maeneo ya jiji na badala yake kuweka meza au miavuli ambazo wataweza kuziondoa wakati wowote  ili kuruhusu matumizi mengine kwenye maeneo waliyojenga vibanda yaendelee.

Akiongea   na Idara ya Habari-MAELEZO, Afisa Mipango miji, Jiji la Dar es Salaam Emmanuel Richard amesema Halmashauri imeanza  kuelimisha  makundi ya wafanyabiashara  wadogo waliojenga vibanda vya biashara pembezoni mwa barabara, kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara pamoja na juu ya mitaro ya maji ya mvua kwani maeneo hayo hayakutengwa kwa matumizi hayo.

“Sheria ya ujenzi mjini na Sheria ya mipango miji hairuhusu kujenga vibanda vya biashara katika maeneo ya waenda kwa miguu  na kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara ikiwa ni pamoja na juu ya mitaro ya maji ya mvua kwani maeneo hayo hayakutengwa kwa matumizi hayo”.

Aidha, amesema, halmashauri inaangalia namna bora ya utekelezaji wake bila kuleta malalamiko huku akisisitiza kuwa ni kosa kisheria kuvamia na kujenga vibanda vya biashara kwenye maeneo yaliyoachwa kwa matumizi ya waendao kwa miguu, chini ya nyaya za umeme na maeneo mengine hatarishi.

Akizungumzia uwezekano wa kuwahamisha, amesema kumekuwa na uhaba upatikanaji wa maeneo yenye miundombinu rafiki kwa wafanyabiashara hao katikati ya jiji hasa ukizingatia ufinyu wa maeneo kulingana na aina ya biashara wanazofanya . 

Ameweka wazi kuwa, mpango wa Halmashauri ya Jiji ni kuwapanga upya wafanyabiashara ndogondogo katika maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo kwani nafasi kama vile masoko ya Karume (Mchikichini), Machinga Complex na sehemu nyingine zitakazopatikana.

Hata hivyo, Richard amesema, mikakati ya halmashauri ni kuendelea kutoa elimu ya maeneo sahihi ya kufanya biashara, kuboresha masoko ya Karume na Ilala ili yaweze kuchukua wafanyabiashara wengi zaidi pamoja na kufufua soko la Machinga Complex ambalo lilijengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao lakini halitumiki ipasavyo.

Pamoja na kuboresha masoko ya pembezoni ili kuvutia wafanyabiashara wengi kutokuvamia maeneo ya mjini, halmashauri inasisitiza wafanyabiashara hao kutumia miavuli au meza zinazoweza kuhamishika wakati wowote maeneo waliyoyavamia yatakapohitajika.

 Ameongeza kusema kuwa, ili kutengeneza mazingira bora ya wafanyabiashara ndogondogo na kuongeza mapato, Halmashauri ya Jiji haina budi kushirikiana na  Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mamlaka ua Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA),Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Umoja wa Wafanyabiashara, Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi zote wezeshi zikiwemo Taasisi za Kifedha.

Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la ujenzi wa vibanda vya wafanyabiasha ndogondogo katikati ya jiji ambavyo vingi vimezuia njia za waenda kwa miguu na kusababisha adha kwa wananchi ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa mazingira.

Mapema Mei mwaka huu, Halmashauri ya Jiji iliwataka wafanyabiashara ndogondogo waliojenga vibanda vyao kwenye maeneo ya hifadhi za barabara na njia za waendao kwa miguu kiviondoa bila shuruti.

Taarifa za maandiko mbalimbali zinaonesha kwamba kwenye oneo moja la wafanyabishara wadogo kumi, 7 kati yao wamejiajiri hasa baada ya Serikali za Awamu ya Tano na Awamu ya Sita kuwatambua wafanyabiashara hao kwa kuwapatia vitambulisho maarufu kama Vitambulisho vya Wamachinga ambavyo vinawaruhsu kufanya biashara sehemu yoyote isipokuwa maeneo ambayo yanazuiliwa kutokana na sababu maalum.

Kuwepo kwa vitambulisho hivyo kumewawezesha wafanyabiashara hao kufanya biashara ndodondogo kwa wingi na kuiwezesha Serikali kupata mapato yake.

Mfanyabiashara ndogondogo aliyejulikana kwa jina la Yarabieli Elibariki ambaye anamiliki kibada cha biashara katikati ya Jiji, ameiambia Habari- MAELEZO kuwa yupo tayari kwenda kwenye maeneo watakayoelekezwa endapo tu maeneo hayo yatakuwa yamekidhi vigezo vya wao kufanya biashara ikiwemo usafiri wa uhakika na mazingira yatakayorahisisha wateja kufika kwa urahisi.

Aidha, mfanyabiashara mwingine mama Ashura anayejishughulisha na biashara ya chakula maeneo ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) amesema, wateja wake wengi ni wanafunzi wa vyuo na baadhi ya wafanyakazi katika ofisi  zilizopo jirani na eneo hilo hivyo ameiomba Serikali iwapatie elimu namna gani wanaweza kuboresha mazingira ya biashara zao.

“ Tunaomba tupatiwe elimu ya namna tutakavyoweza kujenga vibanda ambavyo havitawaletea adha watembea kwa miguu na ambavyo havitaharibu mandhari ya Jiji, endapo tutaelimishwa tutakuwa tayari kufuata maelekezo ili tuendelee kufanya biashara katika maeneo yenye wateja wetu”, amesema mama Ashura.

Mchango wa wafanyabiashara wadogowadogo ni muhimu katika kukuza pato lao binafsi na familia zao pamoja na pato la Taifa. Kutokana na mchango wao, hivyo Halmashauri ya Jiji imeweka mbele mkakati wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao ikiwa ni moja ya mikakati yake katika Awamu hii ya Sita  ili kuwawezesha wafanyabiashara hao  wadogo waendelee kufanya biashara zao pasipo kuvunja Sheria za Mipango miji.

 

Post a Comment

0 Comments