Mawaziri Sadc wapitisha itifaki ya utalii

 


Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) wanaohusika na mazingira, maliasili na utalii wamepitisha itifaki ya utalii ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi hizo.


 Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Juni 19, 2021 naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja  amesema itifaki hiyo imepitishwa kwa lengo la kuimarisha shughuli za utangazaji,  utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi za SADC.


Pia, Mary  amesema Tanzania kama mwanachama wa SADC imekuwa ikishirikiana na nchi wanachama katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na kufanikiwa kudhibiti ujangili.


“Mafanikio yaliyopatikana kutokana na mkakati wa pamoja wa kudhibiti ujangili ni kukua kwa ushirikiano baina ya nchi wanachama katika kudhibiti ujangili na biashara haramu ya nyara na ushirikiano kwenye kutoa mafunzo kwa maofisa wanyamapori kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa rasilimali wanyamapori,” amesema waziri huyo.


Amesema mkutano huo pia umejadili na kupitisha mkakati wa Sadc wa mabadiliko ya tabia ya nchi na mpango kazi wa utekelezaji wake ambapo nchi wanachama zimehimizwa kuutekeleza.


“Ili kuwezesha kutekeleza jukumu la uhifadhi wa mazingira,  mawaziri tumeridhia nchi wanachama wa Sadc kujiunga na mfuko wa mazingira ambapo nchi wanachama zitapata fedha za ufadhili kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi mazingira,” amesema.


Ametaja masuala mengine yaliyojadiliwa katika mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili ni itifaki ya Sadc ya mazingira kwa ajili ya kujenga maendeleo endelevu na mkakati wa misitu wa jumuiya hiyo.

Post a Comment

0 Comments