Jun 20, 2021

Sheikh Uamsho alivyotoa talaka gerezani

  Muungwana Blog       Jun 20, 2021


 Masheikh wa Uamsho, wameendelea kufunguka kuhusu machungu waliyopitia, huku baadhi wakieleza namna wake zao walivyowaomba talaka wakiwa gerezani


Taarifa kutoka miongoni mwao zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa masheikh wanne kati ya 36 waliombwa talaka, huku mmoja aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina akisema baada ya kutoka amebaini aliyekuwa mkewe ameolewa na ana mtoto mmoja.


Masheikh hao waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka 14 walioachiliwa huru kuanzia Juni 15 mwaka huu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwafutia mashtaka yaliyokuwa yakiwaka


Sheikh huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema: “Ilikuwa mwaka jana mke mkubwa alinifuata gerezani, nia ni kuniambia maisha magumu afanyaje? Nilikuwa mpole na kumjibu sina la kusema kwa sababu sijui hatima yangu huku gerezani.”


“Aliniomba ushauri aende wapi nikamwambia sina la kusema pia, basi akaniambia nimpe talaka na nilimpa kwa sababu aliniambia maisha magumu na hajui mimi nitatoka lini gerezani. Juzi nimerudi nikaambiwa ameshaolewa na ana mtoto mmoja.”


Alisema huyo alikuwa mkewe mkubwa ambaye alibahatika kuzaa naye mtoto mmoja, lakini kwa sasa amebaki na mke mmoja ambaye ni mdogo mwenye watoto wawili, huku akitumia nafasi hiyo kumshukuru mke huyo kwa uvumilivu.


“ Namsihi aendelee kunivumilia maana ndio kwanza nimerudi kutoka gerezani. Miaka minane haikuwa mepesi kwa sababu nimerudi nyumba baadhi ya mali zangu nilizokuwa nazitumia kibiashara zote zimeharibika,” alisema.


Mbali na hilo, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa ushirikiano wao uliosaidia kesi yao kuharakishwa kusikilizwa na hatimaye kuachiliwa huru.


Jana aliyekuwa kiongozi wa Uamsho, Sheikh Mselem Ali Mselem aliswali katika msikiti wa Swahaba Mtoni Kidatu, Mjini Unguja huku waumini waliojitokeza katika ibada hiyo wakionyesha furaha yao kwa sheikh huyo.

logoblog

Thanks for reading Sheikh Uamsho alivyotoa talaka gerezani

Previous
« Prev Post

No comments:

Post a Comment