Taasisi za bima ziwe za suluhisho

 


Taasisi za Bima na Fedha, zimetakiwa kuwa mkombozi kwa wafugaji na wavuvi kwa kuhakikisha zinakuwa na uwezo wa kuwa na bima ya mifugo na samaki itakayowasaidia ulinzi wa uwekezaji wao na kuweza kukopesheka.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema hayo, wakati akifungua kikao cha Wadau wa Dawati la Sekta Binafsi ambalo lipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Ulega amesema kuwa wafugaji na wavuvi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kutokopesheka na taasisi za kifedha na hivyo kuwafanya washindwe kuitumia fursa ya mikopo ambayo ipo ili kukuza mitaji yao.

“Kutokana na changamoto hii, wizara imeona ni vema kuwakutanisha wadau wanaohusika ili wote kwa pamoja tujadili tatizo nini, na nini kifanyike ili tutakapotoka hapa tuwe na suluhisho ambalo litajibu tatizo la wafugaji na wakulima kuhusu bima na mikopo,”- amesema Ulega.

Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael amesema dawati lilifuatilia upatikanaji wa bima kwa wafugaji ili kuweza kuwasaidia wafugaji na wavuvi kupata mikopo ambapo Shirika la Bima la Taifa (NIC), limetoa bima kwa vyama vya ushirika vya wafugaji vitatu na vyama vya ushirika vya wavuvi vitatu.

Kikao hicho cha wadau kimehudhuriwa na wawakilishi wa taasisi na kampuni za bima, taasisi za kifedha, wawakilishi wa vyama vya ushirika vya wafugaji na wavuvi pamoja na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Post a Comment

0 Comments