Vipande vinne vya nyumbu vyamtupa jela miaka 20


 Mahakama ya Wilaya ya Serengeti imemhukumu mkazi wa kijiji cha Nyakomogo, Joma Masoya (34) kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumtiwa hatiani kwa kukutwa na vipande vinne vya nyumbu.


Katika hukumu iliyosomwa leo Ijumaa Julai 30, 2021 na Hakimu Mkazi wa Wilaya, Judith Semkiwa katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 55/2020 mshitakiwa ametiwa hatiani kwa makosa matatu aliyoshitakiwa nayo.


Hakimu Semkiwa amesema katika kosa la kuingia kwenye hifadhi bila kibali adhabu yake ni mwaka mmoja, kukutwa na silaha hifadhini adhabu yake ni miaka miwili na kukutwa na nyara za Taifa adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 gerezani.


Mapema mwendesha mashitaka wa Jamhuri, Jakobo Matatala aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa alikamatwa Julai 12, 2020 katika milima ya Kirawila ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kinyume na sheria.


Amesema alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuingia hifadhini bila kibali, kukutwa na silaha za jadi hifadhini bila kibali na kukutwa na vipande vinne ambavyo ni sawa na nyumbu mzima bila kibali na kuomba mahakama kutoa adhabu kali.


Mshitakiwa ameomba apunguziwe adhabu kwa kuwa anategemewa na familia.

Post a Comment

0 Comments