China, Urusi zakasirishwa na mpango wa mkutano wa demokrasia wa Biden


China na Urusi zimeghadhabishwa na mpango wa mkutano wa kidemokrasia uliopangwa na rais wa Marekani Joe Biden ambao hautayashirikisha mataifa hayo huku Beijing ikikasirishwa zaidi na hatua ya kualikwa kwa Taiwan. 


Kualikwa kwa Taiwan na sio China kumesababisha lawama kali kutoka kwa China ambayo inasema inapinga vikali mwaliko huo. 


Hata hivyo, msemaji wa ofisi ya rais ya Taiwan Xavier Chang, amewaambia wanahabari kwamba mwaliko huo ni mageuzi makubwa kwa kisiwa hicho katika wakati China inaendeleza kampeni yake ya kuifanya Taiwan ifungiwe nje ya mashirika ya kimataifa. 


Taiwan imesema kuwa mkutano huo utakuwa fursa adimu kwake kuboresha sifa zake katika jukwaa la dunia. 


Kwa upande wake msemaji wa ikulu ya Kremlin nchini Urusi Dmitry Peskov amesema kuwa mataifa mengi yanapenda kujiamulia yenyewe jinsi ya kuishi na kuongeza kwamba Marekani inajaribu kubinafsisha neno demokrasia. Dmitry amesema kuwa Marekani haiwezi na haipaswi kufanya hivyo.

Post a Comment

0 Comments