Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Polisi kuchunguza kifo cha kigogo Chadema


Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la kifo cha Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kata ya Buswelu mkoani Mwanza, Erasto Makaranga.


 Akizungumza leo Jumatatu Novemba 22, 2021 na Mwananchi kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Ramadhani Ng'anzi amesema maofisa wa jeshi hilo tayari wamefika katika hospitali ya rufani ya mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa mwili wa kiongozi huyo.


"Bado askari wetu wako kwenye eneo la tukio wakiwa wanakusanya ushahidi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa hiyo tusubiri wamalize uchunguzi wao na tukikamilisha tutatoa taarifa," amesema Ng'anzi


Awali, akizungumza na Mwananchi kwa njia simu Msemaji wa familia hiyo, Benjamini Makaranga amesema familia iliapanga kufanya maziko ya mpendwa wao leo Jumatatu Novemba 22,2021 lakini juhudi za kukamilisha mazishi hayo zimegonga mwamba baada ya maofisa wa jeshi la polisi kufika na  kuzuia mwili huo kuchukuliwa kwa uchunguzi zaidi.


"Tumewasili leo asubuhi katika chumba cha hospitali ya rufani ya Sekou Toure kwa ajili ya kuchukua mwili lakini tumezuiwa na watu wa usalama wakidai wanataka kwanza uchunguzi wa mwili ufanyike ndiyo turuhusiwe kuzika," amesema Benjamini


Kwa mujibu wa dada wa marehemu, Macrina Makaranga baada ya familia kubaini kutoweka kwa ndugu yao juhudi za kutoa taarifa katika vituo vya polisi zilifanyika bila mafanikio ndipo walipoamua kutafuta mwili wake katika hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando na hospitali ya rufani ya mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure ndipo walipoukuta ukiwa na majeraha kichwani.


"Tulimtafuta Bugando hatukumpata baadae tukaenda Sekou Toure mara tatu hatukumpata baadae tuliporudi mara ya nne ndiyo tukaukuta mwili wake ukiwa unaonekana una majeraha katika sehemu ya kichwani na mkono wake unaonekana kama umevunjika," amesema Macrina


Erasto Makaranga anadaiwa kutoweka nyumbani kwake Novemba 17 mwaka huu na mwili wake kupatikana Jumamosi Novemba 21,2021 ukiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya rufani ya mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure.

Post a Comment

0 Comments