Rais Samia akumbusha sakata la vifaranga vya Kenya kuchomwa moto

 


Rais Samia Suluhu Hassan amekumbusha sakata la kuchomwa kwa vifaranga vya Kenya vilivyokuwa vikiingizwa na wafanyabiashara nchini, jambo alilosema halikuwa na maana.


Rais Samia ameyasema hayo leo Novemba 28, alipokuwa akizungumza kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uganda lililofanyika jijini Dar es Salaam, akiwa na mgeni wake, Rais Yoweri Museveni aliyekuja nchini kwa ziara ya siku tatu.


Katika hali iliyoonyesha kuzorota kwa uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Kenya, vifaranga zaidi ya 11,000 vilivyoingizwa nchini kutoka nchi hiyo kwa nyakati tofauti vilichomwa moto mwaka 2017.


Kama hiyo haitoshi, Agosti 2020 Tanzania ilizuia safari za ndege za shirika la ndege la Kenya (KQ) baada ya nchi hiyo kuiweka Tanzania katika orodha ya nchi ambazo wananchi wake hawaruhusiwi kuingia nchini kwao kutokana na maambukizi ya Uviko-19.  


Akisisitiza ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Uganda, Rais Samia amesema baada ya mzozo huo, waliyazungumza na hatimaye sasa biashara kati ya Kenya na Tanzania imeimarika.  


“Wafanyabiashara wa Tanzania ni mashahidi, tulikuwa tunavutana hapa na Kenya, kila kinachokwenda hakipiti, hiki akipiti na kule wakizuia na mkuu wa mkoa wetu naye anasema kuanzia leo hakipiti.


“Lakini tulikaa tukaelezana ukweli. Tulikuwa tunachomeana kuku mipakani, dhambi tupu viumbe wa Mungu mnamwaga petrol mnachoma, haikuwa na maana. Lakini tumeondosha vikwazo sasa biashara imekuwa mno. Ukiangalia figure za biashara, Kenya na Tanzania imekuwa mno, tunataka biashara ikakue kwa Uganda pia,” amesema Rais Samia.


Mbali na Kenya, Rais Samia pia alikumbusha jinsi sukari ya Uganda ilivyokataliwa Tanzania.

“Mheshimiwa Rais amesema hapa, aliomba sisi tununue sukari kwake, lakini walisikia statements za Waziri wetu, kwamba hatutanunua, hatutakubali, sasa tha is nonsense (huo ni ujinga). Mheshimiwa Rais tutanunua sukari kutoka Uganda,” amesema.  


Akisisitiza kuhusu uwekezaji, Rais Samia alisema ni lazima uwekezaji huo uendane na maendeleo endelevu ya kiuchumi na mifumo inayoimarishwa katika kujenga uwezo wa uzalishaji wa ndani.


Kuhusu bomba la mafuta, Samia aliwataka wadau kutoka sekta binafsi kutumia fursa zinazopatikana kutokana na utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa serikali za nchi hizo mbili zinafanya jitihada kuhakikisha sekta hiyo na jamii za nchi zote mbili zinanufaika na mradi huo.


"Nitumie nafasi hii kuwaeleza wawekezaji kutoka Uganda kuwa Wizara ya viwanda na biashara kupitia Taasisi yake ya Utafiti na maendeleo ya Viwanda (TIRDO) ina uwezo wa kutoa huduma za kibobezi ikiwemo kufanya ukaguzi katika mabomba ya kuhifadhi na kusafisha mafuta na gesi," alisema Samia


Naye Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kuboresha ushirikiano wake zaidi na si katika siasa na biashara pekee.


Alisema mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi utakuwa na manufaa kwa pande zote mbili na kusaidia kutoa ajira kwa wananchi wan chi hizo.


 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania, Angelina Ngalula alisema katika kongamano lililofanyika juzi walipata maeneo nane ya kufanyia kazi wakati wa utekelezaji mradi huo.

Post a Comment

0 Comments