Vigogo kikaangoni sakata la wamachinga Dar es Salaam

 


Zikiwa zimepita zaidi ya siku 20 tangu wamachinga waanze kuondolewa katika maeneo yasiyo rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema endapo watarejea, watakaochukuliwa ni hatua ni watendaji husika.


Hatua hiyo imekuja baada ya wakuu wa wilaya, watendaji wa kata na mitaa kuingia mikataba na wakurugenzi wa manispaa husika kuhusu utekelezaji wa Kampeni ya Usafi katika Mkoa wa Dar es Salaam.


Makalla alisema hayo jana, alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na kuongeza kuwa, kuna watu wasio waaminifu wanawaambia wafanyabiashara wawape kiasi fulani cha fedha ili waendelee kufanya shughuli zao maeneo yasiyoruhusiwa.


Juzi, Makalla alizindua kampeni ya kudumu yenye kauli mbiu ya “Pendezesha Dar es Salaam” ikiwa na mkakati wa kuhakikisha wamachinga hawarudi kwenye maeneo waliyoondolewa.


Mkakati huo wa usafi utahusisha mtu mmoja mmoja, taasisi za umma na binafsi huku kila mtu akitakiwa kulinda eneo lake kwa kushirikiana na uongozi wa eneo husika.


Hata hivyo, akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, alisema baada ya kuwaondoa wamachinga sasa mji wa Dar es Salaam unapumua na watu wanatembea kwa uhuru tofauti na ilivyokuwa awali.


“Miongoni mwa vikwazo vinavyozuia ufanisi katika kufanya usafi ni ufanyaji holela wa biashara, ikiwamo watu kufanya shughuli kwenye barabara za waenda kwa miguu na mitaro. Sasa baada ya mchakato kukamilika tutapata nafasi ya kufanya usafi kwa ufanisi ili Dar es Salaam iwe safi,” alisema Makalla.


Pia, alisema kila mtendaji kuanzia ngazi ya wilaya hadi mitaa wanatakiwa kusimamia mkakati huo kwa ufanisi.


Mkuu wa mkoa huyo, alisema mkataba huo una malengo mawili ya kudhibiti biashara holela katika maeneo yasiyoruhusiwa sambamba na kuhamasisha watu kufanya usafi.


“Kila mtu asikubali eneo lake kurudi wafanyabiashara. Mfano hapa Mwananchi nje kuna watu (wafanyabiashara) wamerudi, nataka wasirudi, kwa hiyo mtendaji wa mtaa anatakiwa kuwaandikia barua taasisi ya kuhakikisha mnalinda eneo lenu,” alisema Makalla.


“Kama pale vyuo vya IFM na DIT wametoka, nitashangaa kwa nini mtu anakwenda kujenga kibanda wakati uongozi wa vyuo hivyo upo. Tutapita kufanya kampeni ya kuwataka wananchi kurudi katika maeneo waliyopangiwa.”


Makalla alisema mambo hayo mawili yatakuwa ni miongoni mwa vigezo vya kuwapima watendaji kata na mitaa katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuendelea kubaki katika nafasi zao.


Juzi, katika uzinduzi mpango wa kuipendezesha Dar es Salaam, Makalla aliwanyooshea vidole baadhi ya watendaji wanaowahadaa wananchi kwa kuwaambia warudi kwenye maeneo waliyoondolewa na kwamba hawatafanywa jambo lolote.


“Maeneo ya Wazo na Mwenge nawaonya katika hili sitamvumilia mtu, kwa kuwa tunarudishana nyuma badala ya kwenda mbele,” alisema Makalla katika uzinduzi huo.


Hata hivyo, jana akiwa njiani kwenda ofisi za MCL, Makalla alisema alilazimika kusimamisha gari lake mara tatu maeneo ya Daraja la Kijazi Ubungo, baada ya kuwaona watu wakifanya biashara ya kuuza supu barabarani.


“Nilisimama na kuwauliza kwa nini wako pale, wakanijibu wataondoka, nikauliza tena kwa nini mmerudi wakanijibu tutaondoka. Nikapiga simu moja kwa moja kwa Mkuu wa Wilaya wa Ubungo (Kheri James), akasikia wakimwambia kwamba kesho (leo) wataondoka.


“Nikiwa katikati ya daraja, niliona watu wameweka biashara, nikasimama tena, nilipowauliza wakaniambia wanaondoka na kesho (leo) sitawaona. Hii ni kwa sababu kuna ulegevu,” alisema Makalla.


Mbali na hilo, alizitaka manispaa za mkoa huo kusimamia kwa ufanisi sheria ndogo za mazingira pamoja na wenyeviti na watendaji wa mtaa kubeba ajenda ya kuhamasisha usafi katika maeneo yao.


Aidha, Makalla alizitaka kila taasisi kuweka utaratibu wa kufanya usafi kwa jumuiya sanjari na manispaa kuteua makandarasi wenye uwezo watakaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakiwa na watu na vifaa vya kutosha vya kuzoa taka.


Kampeni ya kuipendezesha Dar es Salaam, itahusisha ukarabati wa majengo yaliyopo maeneo mbalimbali ili kuleta mandhari nzuri jijini hapa.


Makalla alisema magari ya kuzoa taka yatakuwa yakikusanya taka kwa wakati kwenye mitaa mbalimbali na kampeni hiyo haitaathiri shughuli nyingine, zikiwamo za kibiashara.


“Naomba wananchi tushiriki kikamilifu usafi wa jumuiya wa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ni jukumu la kila mtu, siyo watu fulani,” alisema Makalla.


Pia, alitaja sababu za Serikali kuja na kampeni hiyo kuwa Dar es Salaam ndio uso na lango la kuingia na kutoka kwa wageni wa mataifa mbalimbali pamoja na wenyeji.


Sababu ya pili Dar es Salaam ni ndio kitovu cha uchumi wa Taifa.


“Sababu nyingine hali ya uchafu wa mazingira ulikithiri, sasa vikwazo tumeshaviondoa na tumekuja na kampeni ya usafi wa mazingira. Kampeni hii itakuwa endelevu itakayohusisha wadau wote muhimu kwa niaba ya wananchi,” alisema Makalla.


Post a Comment

0 Comments