https://monetag.com/?ref_id=TTIb Virusi 10 vya Kompyuta hatari zaidi kuwahi kutokea | Muungwana BLOG

Virusi 10 vya Kompyuta hatari zaidi kuwahi kutokea

 

Virusi vya kompyuta ni tatizo la muda mrefu ambalo limeathiri watu wengi kwa namna moja au nyingine. Inawezekana wewe ni mmojawapo kati ya wale waliowahi kuathiriwa na virusi vya kompyuta; inawezekana pia hujawahi kuathiriwa au hata kusikia swala hili kabisa.

Katika muda ambao Mungu amenijalia kutumia kompyuta (2002 – hadi sasa), nimeshuhudia mengi na kukabiliana na mengi kuhusu virusi vya kompyuta.

Nimewahi kuona watu wakilia kwa kupoteza taarifa muhimu, wengine wakitoa fedha nyingi kutengeneza kompyuta zao zilizoathirika. Mimi mwenyewe nimewahi kuathiriwa mara kadhaa na virusi hivi.

Hivyo basi, hebu leo tutazame virusi 10 vya kompyuta vilivyowahi kutokea ambavyo ni hatari zaidi.

1. Code Red


Kirusi cha Code Red kiliibuka mnamo mwaka 2001 na kubainiwa na wafanyakazi wawili wa eEye Digital Security. Kirusi hiki kiliitwa Code Red kwa sababu wafanyakazi hao walikuwa wanakunywa “Code Red Mountain Dew” wakati walipokibaini.

Kirusi hiki kilipoibuka kililenga seva za Microsoft IIS, na kilijizalisha kwa kiasi kikubwa ili kuteka mfumo mzima wa kompyuta. Kirusi hiki kilisambaa kwa kasi hadi kufanikiwa kuathiri seva za ikulu ya Marekani.

Ndani ya muda usiozidi wiki moja, kirusi hiki kilikuwa kimeshazima seva 400,000 na kompyuta milioni moja duniani kote. Inakadiriwa kuwa kirusi hiki kilisababisha hasara ya takriban dola milioni 2.6 za Marekani.

2. ILOVEYOU

Hiki ni kirusi cha kompyuta kinachoaminika kusababisha athari kubwa sana duniani. Kirusi hiki kilibainika mnamo mwaka 2000 na kuanza kusambaa kwa kasi kubwa kupitia barua pepe.

Inakadiriwa kuwa kirusi hiki kilisababisha athari ya dola zaidi ya bilioni 15, pia inaaminika kuwa asilimia 10 ya kompyuta zote zilizokuwa zimeunganishwa kwenye mtandao duniani ziliathirika.

Kutokana na athari za kirusi hiki, mashirika na taasisi mbalimbali zikiwemo za kiserikali zilizima kompyuta zake ili kukabiliana na kirusi hiki.

3. CryptoLocker

Hiki ni kirusi kilichokuwa kinaathiri kompyuta za Window, kirusi hiki kilificha mafaili ya mtumiaji na kumtaka alipe kikombozi (Ransom) ili apate tena mafaili yake.

Virusi vya aina hii bado vinaendelea kutumiwa na kutengenezwa na wadukuzi duniani. Virusi hivi hudai malipo ya fedha ili kufungua tena mafaili ya mtumiaji; ikiwa hatalipa pesa hizo kwa wakati atapoteza mafaili yake daima.

 4. MyDoom

Hiki ni kirusi kilichoibuka manamo mwaka 2004 na kuathiri kompyuta zilizokuwa zinatumia programu endeshi ya Window; kirusi hiki kilikuwa kikisambaa kwa kasi sana kwa njia ya barua pepe baada ya kile cha ILOVEYOU.

Inaaminika kuwa  kirusi hiki kilitengenezwa na mtu aliyelipwa kwani kilikuwa na maandishi “Andy; I’m just doing my job, nothing personal, sorry,” – (Andy; Ninafanya kazi yangu, hakuna kitu binafsi, samahani)

Inakadiriwa kirusi hiki kilisababisha hasara ya takriban dola bilioni 38.

5. Melissa

Kirusi cha Melissa kilitengenezwa na David L. Smith mwaka 1999. Kirusi hiki kilianza kusambaa kupitia faili la Microsoft word lililokuwa linadaiwa kuwa na nywila (password) za tovuti za ngono. Inadaiwa kuwa mtumiaji alipopakua faili hili na kulifungua ndipo kirusi hiki kilipoingia kwenye kompyuta yake.

Kirusi hiki kilituma barua pepe kwenda kwenye orodha ya watu wote walioko kwenye barua pepe ya mwathirika ili kujisambaza. Kirusi hiki kiliathiri taasisi za kiserikali, benki na hata watu binafsi.

Taasisi mbalimbali za kiusalama zilifanikiwa kumkamata David L. Smith ndani ya kipindi kisichozidi wiki moja tangu kutengenezwa kwa kirusi hiki. Inakadiriwa kuwa kilisababisha hasara ya dola milioni 80.

6. Sasser

Kirusi hiki kiliibuka mnamo mwaka 2004, na kilibuniwa na mwanafunzi wa sayansi ya Kompyuta Sven Jaschan aliyebuni pia kirusi cha Netsky.

Kirusi hiki kiliathiri mfumo wa uwakaji wa kompyuta na kuifanya izime mara kwa mara. Kirusi hiki pia kilijizalisha na kujisambaza kwa kasi kupitia mtandao; inakadiriwa kuwa kilisababisha hasara ya dola bilioni 18.

7. Stuxnet

Inaaminika kuwa kirusi hiki kilitengenezwa na jeshi la Israeli kwa kushirikiana na Marekani, Stuxnet ni mfano wa silaha ya kivita ya kompyuta (Cyberwarfare).

Kirusi hiki kililenga kuathiri mfumo wa kompyuta wa viwandani (Programmable Logic Controller – PLC) wa vinu vya nyukilia vya Iran.

Inadaiwa kuwa kirusi hiki kililenga kuharibu mfumo wa vinu hivyo na kuvifanya viongeze kasi ya utendaji na hatimaye kulipuka. Mfumo uliolengwa ni ule uliotengenezwa na Siemens; hata hivyo baadae Siemens walikabili kirusi hiki.

8. Conficker

Kirusi hiki kinafahamika pia kama Downup au Downadup, kilibainika mnamo mwaka 2008. Kirusi hiki kiliathiri kompyuta kwa njia ya kuifanya iwe botnet. Botnet ni watumiaji bandia wanaotengenezwa ili kufanya uvamizi wa DDoS.

Uvamizi wa DDoS ni udukuzi unaohusisha kuzalisha maelfu au mamilioni ya watumiaji bandia wanaotembelea tovuti fulani kwa wakati mmoja; hili huifanya tovuti husika ishindwe kuwahudumia wote na kusababisha tovuti hiyo isipatikane.

Inakadiriwa kirusi cha conficker kilisababisha hasara ya takriban dola bilioni 9.

9. Zeus

Kirusi hiki kililenga kufanya matendo mbalimbali ya kihalifu kwenye tarakilishi ya mhanga. Kirusi cha Zesus kiliiba taarifa za siri na kumdanganya mtumiaji kufanya mambo mbalimbali ambayo kiuhalisia yangeweka usalama wake hatarini zaidi.

10. Flashback


Kirusi hiki kilichoibuka mnamo mwaka 2011,  hakikuwa maarufu sana lakini kilidhihirisha udhaifu kwenye kompyuta za Mac. Kirusi hiki kilimdanganya mtumiaji kusakinisha (install) programu ya Flash; kisha kuivamia kompyuta yake na kuifanya kuwa botnet.

(Baadhi ya picha ni kutoka tovuti mbalimbali kupitia Hongkiat.com)

Hitimisho

Naamini umestaajabu jinsi wadukuzi na wataalamu wa kompyuta wanavyotumia maarifa yao kutengeneza programu za kutisha. Ni wazi kuwa swala la virusi vya kompyuta limechukua sura mbalimbali hivi leo kama vile kutumika katika maswala ya vita, kutumika kama chanzo cha kipato n.k

Ni muhimu ukafahamu kuwa virusi vipo na ukachukua tahadhari ya kujikinga mapema.


Post a Comment

0 Comments