ACT-Wazalendo chathibitisha uzalendo wake, yatoa wito kwa vijana wajitokeze kuhesabiwa.


Na Ahmad Mmow, Lindi.

Vijana nchini wameombwa washiriki kikamilifu zoezi la sensa ya watu na makazi kwa kujitokeza kuhesabiwa.


Wito huo kwa vijana umetolewa leo mjini Lindi na mwenyekiti wa taifa wa ngome ya vijana wa chama cha Alliance for Change and Transparency- Wazalendo( ACT- Wazalendo), Abdul Nondo alipozungumza na wanachama na wapenzi wa chama hicho wakati wa maadhimisho ya siku ya vijana duniani ambayo chama hicho kitaifa kimeadhimisha katika mkoa wa Lindi.


Akieleza sababu ya kuadhimisha katika mkoa wa Lindi, Nondo alisema vijana wa chama hicho wanatambua kwamba changamoto zinazowakabili vijana wa Lindi zinashabihiana na changamoto za vijana wengine nchini. 


Nondo alisema ACT- Wazalendo kupitia ngome yake ya vijana kinaamini katika nguvu za vijana katika kuchagiza maendeleo ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kwani vijana ni kundi lenye idadi kubwa ya watu nchini.


Alisema ingawa kundi la vijana ni kubwa kwa idadi ya watu lakini ni kundi kubwa lililosahaulika. Huku akisema serikali inatumia takwimu za sensa ya mwaka 2012 ambayo kwa sasa imepita miaka kumi. 


" Kitakwimu, serikali hutumia takwimu za sensa ya 2012 miaka kumi iliyopita inayosema idadi ya watu Tanzania ni  milioni 44.9, asilimia 35. Hizi ni takwimu zisizo na uhalisia kwani ni miaka kumi sasa imepita, idadi ya watu imeongezeka sana," alisema Nondo.


Kwakuzingatia ukweli huo Nondo alitoa wito kwa vijana wajitokeze kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi huu wa Agosti, tarehe 23, mwaka huu wa 2022 ili serikali ipate idadi sahihi ya watu. Wakiwemo vijana badala ya kutumia sensa ya mwaka 2022.


Alisema kwamujibu wa taarifa ya sasa ya shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto( UNICEF) linasema idadi ya wa Tanzania kwasasa ni milioni 60. Ambapo asilimia 70 ya idadi hiyo ni vijana. Ambao wana umri wa kuanzia miaka 18 hadi 40.


Alisema hiyo ni idadi kubwa sana lakini kundi hilo limesahaulika na linaishi katika dimbwi la umasikini ingawa vijana ni nguvu kazi ya taifa kwa asilimia 55.


Nondo aliwaasa vijana wasimame imara kwa kuishinikiza serikali itatue changamoto zinazowakabili katika maisha yao katika nyanja za kiuchumi, siasa, utamaduni na kijamii. Kwani hakuna nchi yoyote duniani iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo bila kuwekeza kwenye kundi la vijana.


Mbali na hayo mwenyekiti huyo wa taifa wa ngome ya vijana aligusia suala la baraza la vijana la taifa kwa kusema baraza la vijana ndicho chombo kitakachowaunganisha vijana nchi nzima bila kujali itikadi za kisiasa. Ambalo litaratibu fursa kwa vijana na utatuzi wa changamoto zinazo wakabili kuanzia ngazi za chini hadi kitaifa.


Alisema pamoja na umuhimu na faida kubwa ya baraza hilo kwa vijana lakini mchakato wa kuundwa kwa baraza hilo unachukua muda mrefu kukamilika ingawa sheria namba 12 ya baraza la vijana ya mwaka 2015 ipo lakini mchakato  haujakamilika.


" Haileweki kwanini baraza hilo halijaundwa. Sababu zinazotolewa na serikali ni nyingi. Kwamba kanuni hazijasainiwa na waziri husika, mara kuna mchakato wa kuunda kanuni za baraza. Tangu mwaka 2015 hadi sasa2022 ni miaka nane imepita lakini tunaambiwa lipo kwenye mchakato" karibu nchi zote za Afrika Mashariki zinamabaraza ya taifa ya vijana na sasa kuna mchakato wa kuunda baraza la vijana la Afrika Mashariki," alisisitiza Nondo.


Nondo pia alizungumzia suala la sera ya maendeleo ya vijana. Ambapo alisema maendeleo na ustawi wa vijana nchini ni jambo linalotegemea nchi kuwa na sera bora ya vijana inayotekelezeka na kutoa miongozo kwa ajili ya utekelezaji. Hata hivyo sera iliyopo ni ya mwaka 2007 ingawa kuna mabadiliko makubwa yametokea.


Kuhusu katiba mpya Nondo alisema yanahitajika maridhiano ya kitaifa ili ikiwezekana  kufanyike muendelezo wa rasimu ya katiba ya tume ya Warioba.

Post a Comment

0 Comments