Benki ya NBC yasisitiza dhamira yake ya kukuza sekta ya michezo, sanaa na utamaduni



Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza kuhusu adhma yake ya kukuza na kuendeleza sekta ya michezo hapa nchini kwa kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo inayokua kwa kasi.

Akizungumza kwenye hafla ya jioni iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ikilenga kuwapongeza na kuwakaribisha wanamichezo wa Kitanzania walioshiriki kwenye Mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika hivi karibuni Birmingham, Uingereza, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw. Theobald Sabi alisema sekta ya michezo, sanaa na utamaduni ina mchango muhimu katika suala zima la ajira pamoja na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na pato la taifa kwa ujumla.

“Pamoja na kuitikia wito wa serikali katika kuinua sekta hii muhimu, benki ya NBC tumebaini kwamba sekta hii ni eneo la kimkakati kiuchumi iwapo sisi kama wadau muhimu tutaiunga mkono,’’ alisema Bw Sabi kwenye hafla hiyo iliyohudhuliwa na wadau mbalimbali wa sekta hiyo wakiwemo viongozi waandamizi wa serikali  wakiongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Bw Sabi alibainisha kuwa benki hiyo Ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na wadau wa sekta michezo, sanaa na utamaduni na dhamira hiyo inapimwa kwa namna ambavyo taasisi hiyo hiyo inadhamini matukio mbalimbali ya kimichezo hapa nchini ikiwemo Ligi Kuu  ya Tanzania Bara (NBC Premier League), NBC Dodoma Marathon, mashindano mbalimbali ya mchezo wa golf pamoja na kuunga mkono jitihada za ujenzi wa miundombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa viwanja vya mpira katika maeneo mbalimbali nchini.

“Hivyo basi kwetu NBC milango ipo wazi wa wadau mbalimbali wa sekta ya michezo, sanaa na burudani ili tuweze kushirikiana katika kukuza sekta hii muhimu lengo likiwa ni kukuza ajira ambayo ni nyenzo muhimu kiuchumi na ustawi wa sekta ya fedha nchini,’’ alisema.


Pamoja na kuwapongeza na kuwakaribisha wanamichezo wa Kitanzania walioshiriki kwenye Mashindano ya Jumuiya ya Madola hafla hiyo pia ilihusisha makabidhiano ya taarifa ya namna bora ya kusimamia HAKIMILIKI na ugawaji wa Mirabaha kwa wamiliki wa kazi za sanaa nchini.

Post a Comment

0 Comments