Matokeo ya awali :Odinga wa Kenya yuko mbele kidogo katika kinyang'anyiro cha urais


Aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga yuko mbele kidogo katika kinyang'anyiro cha kuwania urais dhidi ya Naibu Rais aliye madarakani William Ruto kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyoonyeshwa jana.


Kulingana na takwimu zilizotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Odinga ana asilimia 52.54 ya kura dhidi ya asilimia 46.76 ya Ruto, baada ya takriban asilimia 30 ya fomu kutoka vituo vya kupigia kura kujumuishwa. 


Tume ya uchaguzi siku ya Ijumaa ilikiri kuwa shughuli ya kujumuisha kura ilikuwa ikienda polepole sana na kuomba taifa kuwa na subira. Aidha tume hiyo ilikanusha kuwa tovuti yake ya matokeo ilikuwa imedukuliwa na kusisitiza kuwa mifumo yake ilikuwa salama.


Uchaguzi huu unaonekana kuwa mtihani wa uthabiti wa mamlaka katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ambalo chaguzi zake zilizopita ziligubikwa na shutuma za wizi wa kura na ghasia.

Post a Comment

0 Comments