https://monetag.com/?ref_id=TTIb MABANDA BORA YA KUKU | Muungwana BLOG

MABANDA BORA YA KUKU

Ujenzi wa mabanda bora ya kuku ni miongoni mwa mambo ya msingi kabisa katika ufugaji bora wa kuku wawe ni wa asili au wale walioboreshwa. Hata hivyo si kila mtindo wa ujenzi unafaa, kwahiyo ujenzi huo ni lazima uzingatie mahitaji halisi ili ufugaji huo uweze kutoa matokeo bora yanayotarajiwa na mfugaji.


Mambo muhimu katika ujenzi wa banda la kuku ni;

  1. Liingize hewa safi wakati wote.
  2. Liwe kavu daima.
  3. Liwe nafasi ya kutosha.
  4. Liwe la gharama nafuu lakini la kudumu.
  5. Lizuie kuingia wanyama na wadudu hatari kwa kuku.
  6. Liwe na nafasi ya kuweka vyombo vya chakula na maji.
  7. Lizuie upepo wakati wa baridi kali.


HEWA NA MWANGA:
Hewa ni muhimu kwa kila kiumbe, hivyo banda la kuku ni lazima liingize hewa safi na kutoa ile chafu na liweze kuingiza mwanga wa kutosha.

  1. Kwa kifupi ni kwamba madirisha ya banda ni lazima yawe makubwa na ya kutosha ili yaingize hewa safi na kutoa ile chafu.
  2. Ni vema madirisha haya yawe juu kiasi cha meta moja (1) kutoka chini ili hewa ipite juu ya vichwa vya kuku.
  3. Hewa safi siyo upepo, hivyo jaribu kuzuia upepo mkali kuingia ndani ya banda la kuku ama sivyo kuku wataugua ugonjwa wa mafua na niumonia na vifaranga vinaweza kufa  kwa ugonjwa wa baridi.
  4. Jenga   Banda lako kwa kukinga upepo unakotokea na kupanda miti kuzunguka banda hilo la kuku ili kupunguza kasi ya upepo na kuweka kivuli dhidi ya jua kali na joto.



UKAVU NA USAFI WA NDANI:
Kwa vile kuku si ndege wa majini kama bata , ni jambo la busara kuhakikisha kuwa mahali anapoishi hapana unyevunyevu.

  • Banda la kuku lijengwe mahali palipoinuka ili kuzuia maji ya mvua yasiingie.
  • Wajengee kuku uchaga wa kulalia kwa kuweka viguzo vyenye urefu wa meta moja na kutandika miti juu yake ili usiku walale hapo, kuliko kuwalaza ardhini au sakafuni.
  • Ukavu wa banda ni muhimu sana hasa kwa vifaranga na kuku wanaotaga. Ndani ya banda lenye unyevu mayai kuchafuka sana hata wakati mwingine huoza kwa urahisi na jitihada zako zitakuwa ni bure.
  • Sakafu ya banda ni vizuri ikawa ya zege lakini kutokana na uhaba wa fedha sakafu inaweza kutengenezwa kwa mabanzi (mabanda yaliyoinuliwa) au udongo mgumu na au mchanga ambao utafunikwa kwa mabaki ya taka za mpunga na yale ya mbao. 
  • Ili kuepuka unyevunyevu ni vyema eneo/mahali pla kujenga banda pawe pameinuka na penye kupitisha hewa ya kutosha.


PAA LA BANDA:
Paa la banda liwe madhubuti ili kuzuia maji ya mvua kuingia hasa wakati wa masika. Sakafu ya banda iwe juu zaidi ya usawa wa nje. Paa linaweza kuezekwa kwa mabaki ya vipande vya bati , madebe na kama ikishindikana tumia nyasi zinazofaa kwa ajili ya kuezeka nyumba katika eneo hilo.

NAFASI YA KUFANYA KAZI:
Banda la kuku lisiwe na nguzo au mbao nyingi sana ndani kiasi cha kumfanya mhudumiaji wa kuku ashindwe kufanya kazi zake. Hali hiyo itamfanya apoteze muda mwingi katika kuzizunguka nguzo hizo, hasa wakati wa kuokota mayai au kufanya usafi.

VIFAA:
Unapotaka kujenga banda la kuku kwanza kabisa tayarisha vifaa vinavyotakiwa. Vitu kama miti au nyasi, nyavu au fito, misumari au kamba ni muhimu kuviandaa mapema.
Pili ni lazima uwe na plani/ramani kamili ya banda hilo. Kwa wastani kila kuku anahitaji nafasi ya Meta za eneo la 0.11 hadi 0.22 (futi 1 hadi 2 za eneo.) kutegemeana na umri wa kuku.

UJENZI RAHISI:
Kuku wafugwao hatimaye ni lazima wafidie gharama za Ujenzi wa mabanda na chakula. Gharama zikiwa kubwa sana huenda ukaifanya shughuli ya ufugaji isiwe na faida hata kidogo hali hiyo itamfanya mfugaji aone ufugaji hauna maana yoyote kwake. Lakini ukijenga banda lako kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi utaongeza faida zaidi kwakuwa umepunguza gharama za uendeshaji wa mradi.

VIPIMO:
Banda la kuku linatakiwa liwe na Meta 15 hadi meta 22 za eneo yaani Meta 3 hadi 4.5 za upana kwa meta 5 za urefu. Banda hili linaweza kutunza kuku 100 wakubwa kwa wakati mmoja.

HITIMISHO;

  • Ujenzi wa mabanda unasisitizwa katika kuboresha ufugaji wa kuku wa asili ili;
  • Kuongeza uzalishaji na kupunguza vifo vya vifaranga kwa majanga mbalimbali kama vicheche ,mwewe, mapaka, mbwa na wizi wa kuku wanaozurura holela.
  • Vile vile inatarajiwa kwamba kuku wanaozuiliwa kwenye banda na kuwekewa chakula mchanganyiko wataongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.