Mashabiki Simba Vs Yanga watakiwa kutii sheria

Jeshi la Polisi limewataka mashabiki wa soka nchini kuzingatia sheria bila ya shuruti katika mpambano wa watani wa Jadi Simba dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro amesema, wamejipanga kuhakikisha amani inakuwepo kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa mchezo na kuhakikisha kila mwananchi anaondoka akiwa salama.

Sirro amesema, wamejipanga pia kuzuia waharibifu wa miundombinu ya uwanja kuanzia mwanzo wa mchezo mpaka mwisho huku akiwataka mashabiki kuzingatia utaratibu uliotolewa juu ya upatikanaji na matumizi ya tiketi za kielektroniki zitakazoanza kutumika katika mchezo huo.

Sirro amesema, wanashirikiana na Shirikisho la Soka nchini ili kuhakikisha mashabiki wanaingia uwanjani kihalali kwa kutumia tiketi zilizohalalishwa.

Bora Shilole kuliko Petit Man - Nuh Mziwanda

Msanii wa Bongo Fleva Nuh Mziwanda kwa sasa ameingia katika mgogoro na aliyekuwa meneja wake, Petii Man kutokana na madai kuwa Petii Man amekuwa akitumia jina lake vibaya kupiga hela.

Nuh alitumia dakika 4 akiiambia eNewz kuwa Petii Man alikuwa ni mpigaji, na hakuwa na mchango wowote katika kuuendeleza muziki wake, huku akimkumbuka mpenzi wake wa zamani kwa kusema "Mtu wa kumshukuru katika muziki wangu ni Shilole na si Petit Man".

Nuh aliongeza “Nilishapoteza miaka mitatu kwa ishu za mapenzi sasa siwezi kupoteza mwezi mmoja kwa mtu ambaye hana mchango wowote kwangu na kanikuta tayari nimeshakuwa star, siwezi kufanya kazi na yeye kwa sababu hatuendani na anachukua hela kupitia mgongo wangu bila mimi kujua na pia ni meneja ambaye yeye anahangaika zaidi yeye mwenyewe kuwa star".

Pia Nuh alitambulisha Studio yake mpya aliyoipa jina la L.B RECORDS huku akijibu watu wanaosema kuwa studio hiyo ndiyo imefanya angombane na meneja wake (Petii Man) kwa kusema "studio hii ni jasho langu na haihusiani na ugomvi wetu".

Wanyonge, maskini waathiriwa na uhaba wa dawa

Dar es Salaam. Serikali imeshauriwa kulitazama suala la uhaba wa dawa nchini kama janga la Taifa.

Kwa muda sasa kumekuwapo madai ya uhaba wa dawa nchini, jambo ambalo wadau wa afya, wanasiasa na wanazuoni wanaeleza linawaumiza Watanzania wanyonge na maskini.

Hata hivyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilikanusha taarifa za uhaba huo na kusisitiza kuwa zilizopo zinatosha kwa asilimia 53.

Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe amesema tatizo la dawa ni kubwa kuliko watu wanavyodhani. Amesema ufisadi wa Sh850 bilioni wa ‘Akaunti ya Tegeta Escrow’ ni zaidi ya mara tatu ya bajeti yote ya dawa kwa mwaka.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana amesema ukosefu wa dawa nchini ni janga kama watoa takwimu hawazitoi kwa usahihi.

Mwanasheria maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari ameitupia lawama Serikali kwa kushindwa kulinda vyanzo vya fedha na kusababisha kuwa na bajeti ndogo ya afya.

Tasaf yawezesha miradi ya ufugaji

Bukombe. Baada ya kunufaika na fedha za ruzuku za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wakazi wa Kata ya Busonzo wilayani hapa Mkoa wa Geita, wameamua kuwekeza katika miradi ya ufugaji.

Mkazi wa Kijiji cha Nampalahala, Monica Mwombeki, amesema amekuwa akipokea Sh36,000 kila baada ya miezi miwili.

Amesema ameshapokea fedha hizo kwa awamu nane na zimemsaidia kufuga kuku hivyo kujiongezea kipato. Anatarajia kuwekeza katika ufugaji wa mbuzi, kondoo na kuku ili kuondokana na umaskini wa kipato.

Barabara za TAMISEMi zaongezewa fedha hadi bil 247

Waziri wa nchi, ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene mesema serikali imetenga shilingi bilioni 247.6 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zilizo chini ya TAMISEMI.

Amesema kiasi hicho ni mara 10 ya fedha ambazo zilikuwa zikitengwa awali ili kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ambayo huzalisha malighafi mbalimbali zinazohitajika viwandani.

Mhe. Waziri Simbachawene ameyasema hayo kwenye mkutano watano kati ya TAMISEMI, Bodi ya Mfuko wa Barabara na wadau wa wakala wa Serikali za Mitaa.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa barabara hizo serikali imeongeza fedha hizo kutoka shilingi Bilioni 23.8 za mwaka wa fedha 2015/2016 hadi shilingi Bilioni 247.6 kwa mwaka huu ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Aidha, amewaonya wakurugenzi wanaochelewesha kwa makusudi malipo kwa wakandarasi kuacha kufanya hivyo mara moja kwani vitendo hivyo vinachangia kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwamba mtu atakaye bainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Wasanii wa singeli tupunguze usela - Chokoraa

Mkali wa kurap na kuimba kutoka bendi ya Twanga Pepeta Khalid Chokoraa ameamua kuingia kwenye muziki wa kisingeli huku akiwataka wanamuziki wa kisingeli nchini kuacha kuuchukulia muziki huo kama ni wa kihuni.

Akipiga story ndani ya eNewz, Chokoraa amesema "Kikubwa zaidi nawasihi wasanii wa kisingeli kuangalia maneno wanayoyatumia na kupunguza maneno ya mtaani ili tuelimishe kupitia kisingeli".
Chokoraa alisema wasanii wa kisengeli ambao anatamani kuimba nao ni Sholo Mwamba, Man fongo na Makabila, na kwamba anatarajia kuachia video yake Jumatatu ya wiki hii na kuwataka mashabiki zake kuisubiri kwa hamu kwa kuwa wimbo huo unaelimisha, unaburudisha na una ujumbe mzuri kwa jamii.

Chadema kuahirisha tena Ukuta?

KESHO Ijumaa ya tarehe 30 Septemba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huenda kikatangaza kuahirisha tena uzinduzi wa operesheni iliyobatizwa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta)

Uzinduzi wa operesheni Ukuta, ulitangazwa tarehe 27 Julai mwaka huu na kwamba ungefanyika mnamo Septemba Mosi, mwaka huu hata hivyo uliahirishwa siku moja kabla ya kufanyika kwake kutokana na kile kilichoitwa, ‘ombi la viongozi wa dini’.
“Tunatangaza kuahirisha mikutano na maandamano ya Ukuta kwa kuwa viongozi wa dini, wametuomba tuwape angalau wiki tatu ili wafanye mazungumzo na Rais John Magufuli ili kutafuta suluhu ya suala hili na kama ikishindikana basi tutaifanya Oktoba mosi mwaka huu,” alisema Freeman Mbowe Agosti 31, mwaka huu.

Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni.
Hata hivyo, wiki iliyopita Salum Mwalimu, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, alipoulizwa  kuhusu uzinduzi wa operesheni hiyo hasa ikizingatiwa kuwa zimebaki siku chache kabla ya Oktoba Mosi, alijibu kuwa, “Ukuta siyo tarehe.”

“Ukuta ni fikra zinazoishi ndani ya mioyo ya watu na zitaendelea kuishi. Suala siyo kubaki kwa siku tano au kumi. Tunasubiri tupate mrejesho kutoka kwa viongozi wa dini halafu tutafanya uamuzi juu ya suala hilo,” alisema.

Tumaini Makene, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, ametoa taarifa jioni ya leo akisema, chama hicho kitatoa tamko juu ya suala hilo siku ya kesho.

“Taarifa rasmi kuhusu Ukuta na hatima ya siku ya maandamano na mikutano nchi nzima iliyotangazwa na chama, itatolewa kesho Ijumaa, Septemba 30, 2016, saa 5:00 asubuhi, mzungumzaji mkuu atakuwa ni Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama Taifa,” amesema Makene.

Dalili za awali zinaonyesha kuwa, Chadema inaweza kuahirisha tena kufanyika kwa uzinduzi wa operesheni hiyo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuchelewa kupata majibu ya viongozi wa dini juu ya jaribio lao la kuonana na Rais John Magufuli ili kutafuta suluhu.

Taarifa zaidi zinadai kuwa, mpaka sasa jaribio la viongozi wa dini kuonana na Rais Magufuli na kujadili suala la kuruhusu kufanyika kwa mikutano na maandamano nchi nzima limegonga mwamba.
Pia chama hicho kinaonekana kutofanya maandalizi yoyote ya msingi kulinganisha na joto la maandalizi lililokuwepo kuelekea uzinduzi wa operesheni hiyo Septemba Mosi mwaka huu kabla ya kuahirisha.

Itakumbukwa kuwa, wiki mbili zilizopita, gazeti moja la kila siku liliripoti kuwa Rais Magufuli amekataa kuonana na viongozi wa dini ili kuzungumzia suala la Ukuta.

Habari ya gazeti hilo ilikuwa na kichwa cha habari, “Rais Magufuli awatosa viongozi wa dini.”
Vuguvugu la uzinduzi wa operesheni Ukuta mwezi uliopita, lilisababisha jumla ya wanachama na viongozi wa Chadema 230 kukamatwa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na wengine 28 kushikiliwa mahabusu mpaka tarehe 1 Septemba ilipopita.

Lulu Diva Amdhalilisha Tiffah Wa Diamond

Video queen matata Bongo, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’ anadaiwa kumdhalilisha mtoto wa Mbongo Fleva anayefanya vizuri kwa sasa, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Latifa ‘Tiffah’ kwa kumuita mbwa wake jina Shikiki, ambalo pia ni jina jingine la utani la mtoto huyo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, mrembo huyo amemuita mbwa wake huyo jina hilo, kitu ambacho kimetafsiriwa na wengi kama ni kumdhalilisha mtoto huyo wa staa mkubwa Bongo.

“Jamani Diva anatafuta matatizo makubwa na D i a m o n d , kwanini kampa mbwa wake jina kama hilo ambalo pia huwa linatumiwa na Tiffah? Ana hatari sana,” kilisema chanzo chetu.

Gazeti hili lilipomtafuta Lulu na kumuuliza kuhusu ishu hiyo, alisema ni kweli mbwa wake anaitwa Shikiki lakini hakuwa akijua kwamba mtoto wa Diamond, jina lake lingine ni hilo.

“Jamani mimi sikuwa najua kabisa kama Tiffah, jina lake lingine ni hilo, mimi nilimpa tu kama watu w e n g i n e wanavyowapa m a j i n a mbwa wao,” alisema Diva.

Mashabiki wa mpira wajitokeza kuchukua kadi za kieletroniki.

  Moja ya kadi za kieletroniki.

Mashabiki wa Mpira wakiwa wamepanga foleni ya kwenda kukata tiketi za kieletroniki jijini Dar es Salaam leo.

MFUMO mpya wa kadi za kieletroniki umeonekana kupokelewa kwa mwitikio mkubwa sana na wananchi wengi kujitokeza kupata kadi zitakazowawezesha kukata tiketi kwa njia ya kuingia uwanjani kuangalia mpira.

Katika maeneo mbalimbali kadi hizo zimekuwa zikitolewa kwa shilingi 1000 hadi 3000 zimekuwa chachu ya serikali kupata mapato halisi tofauti na ulivyokuwa mfumo wa tiketi za kawaida na utatakiwa kuisajili kwa jina lako la kwenye kitambulisho cha kupigia kura sambamba na namba ya simu unayoitumia na utatakiwa kujaza fedha na kulipia kulingana na sehemu unayotaka kwenda kukaa.

Mfumo huo rasmi unaanza kutumika Oktoba 01 kwenye mchezo baina ya Yanga na Simba na utamlazimu mwananchi au shabiki anayetaka kushuhudia mchezo huo kuwa na kadi maalumu atakayotumia kuingilia mlangoni na kumuonyesha ni mahala gani anatakiwa kwenda kukaa

Kuja kwa mfumo huo timu mbalimbali zitaacha kulalamika kuhusiana na tiketi feki zilizokuwa zinauzwa na watu wasiojulikana na kuhujumu mapato ya timu zao.

ICC kuchunguza ghasia nchini Gabon

Mwendesha mashtaka wa mahakama kuu wa kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC) Fatou Bensouda, anasema kuwa anafuatilia ghasia zinazoendelea nchini Gabon kufuatia utata uliokumba uchaguzi wa rais.

Serikali ya Gabon imeomba ICC kufanya uchunguzi ikiwalaumu wafuasi wa kiongozi wa upinzani Jean Ping kwa kuchochea mauaji ya halaiki na uhalifu mwingine dhidi ya binadamu.

Wafuasi wa upinzani walichoma bunge baada ya rais Bongo kutangazwa mshindi kwenye uchaguzi huo wa Agosti 27, huku naye Ping akisema kuwa makao makuu ya chama chake yalipigwa bomu.